Habari za Punde

JK Aonesha Picha za Wazazi Wake

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akionesha picha ya mama yake mzazi
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akionesha picha ya mama yake mzazi
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akionesha picha ya Baba yake Mzazi  Mzee Kikwete Mrisho Kikwete a.k.a Khalfani Mrisho Kikwete

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akionesha picha ya Babu yake Mzaa baba  Chifu Mrisho Kikwete.


Na Issa Michuzi

Akiwa katika mahojiano katika kipindi maalumu cha kuadhimisha miaka 72 ya kuzaliwa cha  JK72 na watangazaji wa Clouds FM na Clouds TV, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mkewe Mbunge wa Mchinga Mhe. Mama Salma Kikwete alitumia wasaa huo kuonesha picha za wazazi wake, ikiwa ni pamoja na za Babu yake mzaa baba, Baba Mzazi na Mama Mzazi.

 

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika kijijini Msoga IJUMAA OKTOBA 7, 2022 Dkt. Kikwete alisimulia kwamba Babu yake Mzee Mrisho Kikwete alikuwa Chifu wa Wakwere na kwamba baba yake mzazi Mzee Kikwete Mrisho Kikwete au kwa jina lingine Khalfani Mrisho Kikwete alikuwa Mkuu wa Wilaya PanganiSame na Tanga katika vipindi tofauti tofauti. Alisimulia kwamba  wakati mama yake alipokuwa mja mzito naye, babu alitamka kuwa ikiwa mtoto atakuwa wa kiume atampatia urithi wa cheo chake, cha Uchifu.

 

Historia fupi ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ni kwamba alizaliwa tarehe 7 Oktoba mwaka 1950 katika kijiji cha Msoga, mkoa wa Pwani, akiwa mtoto wa sita katika familia ya watoto tisa. Alimuoa mama Salma Kikwete mwaka 1989 na wamebarikiwa watoto nane.


Alipata elimu ya msingi na ya kati katika shule za Msoga na St. John Bosco Lugoba kati ya mwaka 1958 na 1965. Aidha, alipata elimu ya sekondari katika shule za sekondari za Kibaha (1966 – 1969) na Tanga (1970 – 1971). Alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1975 na kupata Shahada ya Uchumi, 

Mwaka 1976 alijiunga na Chuo Kikuu cha Maofisa wa Jeshi Monduli na kutunukiwa Cheo cha Luteni Kanali na baadaye kuwa Mkufunzi Mkuu na Kamisaa wa Siasa katika chuo hicho. Mheshimiwa Kikwete amefanya kazi katika Chama cha Mapinduzi kwa nyadhifa mbalimbali kwenye mikoa ya Singida na Tabora na  wilaya za Nachingwea na Masasi.

 

Mwaka 1988 aliteuliwa kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Mwaka 1990 alichaguliwa kuwa mbunge wa  Jimbo la Bagamoyo na akateuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini. Nyadhifa nyingine alizoshika ni Waziri wa Fedha mwaka 1994 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.


Alishika rasmi wadhifa wa urais mwaka  2005 na kuchaguliwa tena 2010 kwa muhula mwingine wa  miaka mitano.

 

Mengine, kama wanavyosema, ni historia. 

 

Katika kumalizia mahojiano hayo Dkt. Kikwete alibainisha kwamba yuko katika hatua za mwisho mwisho kukamilisha kuandika kitabu cha maisha yake ambacho amesema kitakuwa na kila kitu kinachomhusu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.