Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto bi Abeida Rashid Abdallah amesema Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kusaidia maendeleo ya jamii hasa wenye mazingira magumu na wasiojiweza ili kuwapunguzia ukali wa maisha.
Akizungumza baada ya kuwakabidhi msaada wa chakula mbali mbali kwa watu wenye mazingira magumu Wajane, Wazee wasiojiweza, watu wenye ulemavu na Watoto Yatima huko Kidimni, amesema kuna baadhi ya Watoto wanaishi katika mazingira magumu hivyo michango na misaada mbalimbali inahitajika ili kuwasaidia watu hao.
Amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mianya hiyo ya kutoa misaada na hatimae kuwafanyiwa vitendo vya udhalilishaji watoto na hata wazee, jambo ambalo linaleta athari kubwa katika jamii.
Hivyo amesema ni vyema jamii pamoja na Jumuiya mbalimbali kushirikiana na Wazee na Wizara wanapohitaji kutoa misaada ili kusaidia kupunguza vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia katika jamii.
Hata hivyo bi Abeida ameishukuru Jumuiya hiyo ya Good People Hope Box kwa kutoa msaada huo wa chakula na kuwaomba kuendelea kusaidia Jamii kama hiyo ili kusaidia kuwapunguzia ukali wa maisha.
Nao waanzilishi wa Jumuiya ya Good People Hope Box, bibi Mi Sook Chol pamoja na mumewe bwana Kwan I'il Park wamesema wamekuwa wakisaidia kutoa huduma katika Jumuiya mbali mbali kwa lengo la kupunguza ukali wa maisha kwa watu wasiojiweza, wenye mazingira magumu, watu wenye ulemavu pamoja na Watoto Yatima ili kuwapunguzia ukali wa maisha.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya Wazee ndugu Amani Suleiman Kombo kwa niaba ya wazee wezake ametoa shukurani kwa msaada waliopatiwa na kuomba wasichoke kutoa kila watakapojaaliwa.
Msaada uliotolewa ni pamoja na Mchele, Sukari, unga wa sembe, mafuta ya kupikia,chumvi, sabuni ya kufulia, pamoja na msuwaki na dawa ya meno.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment