Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk Shein aongoza kikao cha NEC Zanzibar

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein (wa pili kulia),akiongoza Kikao Maalum Cha Halmashsuri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Hemed Suleiman Abdulla pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi (wa kwanza kulia) wakiwa katika kikao hicho kilichofanyika leo Novemba 29, mwaka 2022 Kisiwandui Unguja

Na.Is-haka Omar - Zanzibar.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimekamilisha mchakato wake wa ratiba za Uchaguzi kwa ngazi ya Taifa kwa upande wa Zanzibar.

 

Mchakato huo unakamilika kupitia Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar  kilichokaa leo tarehe 29/11/2022  kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.

 

Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi Kuu ya CCM,Kisiwandui Zanzibar.

 

Pamoja na mambo mengine Kikao kimepokea mapendekezo ya majina ya WanaCCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Viti 15/20 vya Zanzibar kutoka katika Mikoa sita ya Kichama.

 

Kupitia kikao hicho kimepokea na kujadili taarifa mbili ambazo ni taarifa ya awali ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Amani, pamoja na Taarifa Maalum ya Maadili kwa wajumbe..

 

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Viti 15/20, lilifanyika kwa wakati tofauti kuanzia tarehe 02/7/2022 hadi zoezi la mwisho la tarehe 05/10/2022.

 

Jumla ya Wana CCM 598 Wanaume ni 353 sawa na asilimia 59 na Wanawake ni 245 sawa na asilimia 40.96 wajimejitokeza kuomba kuteuliwa nafasi hizo kwa upande wa Zanzibar.

 

Katika kujadili na kufanya uchambuzi kwa walioomba, Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar ilizingatia sifa kwa mujibu wa Ibara ya 17 na 18 za Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 Toleo la 2022 inayoeleza sifa na miiko ya viongozi wa CCM.

 

Sambamba na hayo kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za CCM kifungu cha 102 kinaeleza kwamba “ kwa upande wa Zanzibar , mapendekezo ya Kamati za Siasa za Mkoa juu ya waombaji wa nafasi hii yatawasilishwa kwenye kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo itawafikiria na kutoa mapendekezo yake kwenye Kikao cha Kamati Kuu’’

 

Katika kifungu cha 103 kinafafanua kwamba “ Kamati Kuu itachunguza sifa za waombaji wa nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa pamoja kutoa Bara na Zanzibar na kuwasilisha mapendekezo yake juu ya waombaji wote kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa.

 

Pia kifungu cha 104 kinaeleza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa itawafikiria waombaji hawa na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa nafasi hizi.

 

Viongozi mbali mbali walioudhuria kikao hicho ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeil Ali Maulid pamoja na Wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.