Habari za Punde

Mhe.Chande Aitaka TIRA Kudhibiti Kampuni za Bima Zinazofanya Ubabaishaji

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (kulia), akioneshwa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema (wapili kulia), mabanda mbalimbali yaliyopo katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yanayoendelea katika Viwanja vya Rock City Mall, jijini Mwanza.

Na Farida Ramadhani, WFM, Mwanza

Serikali imeiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) kuzichukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuzifutia leseni za kufanyabiashara nchini kampuni za Bima zinazoshindwa kutekeleza wajibu wao wa kuwalipa wateja wao fidia za majanga mbalimbali kwa wakati na kwa kuzingatia thamani halisi ya mali zilizokatiwa bima husika. 

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipotembelea na kukagua mabanda ya waoneshaji katika maadhimisho ya pili ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Rock City Mall, jijini Mwanza.

Alisema wahanga wamekuwa wakipata usumbufu wakati wa kudai fidia kwa kuwa hawalipwi kwa wakati na hata ukifika muda wanapolipwa fedha inakuwa imeshashuka thamani.

“Malalamiko mengi yamekuja Wizarani kuhusu kampuni hizo za bima, naiagiza TIRA izichukulie hatua kampuni zote ambazo hazifuati sheria na taratibu”, aliagiza Mhe. Chande.

Aliiagiza pia ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima kutoa suluhu kwa wakati na kwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali ya nchi na kuhakikisha kuwa kampuni za bima zinawajibika ipasavyo kwa matendo yao ili kuwawezesha wahusika kupata haki zao kwa wakati.

Aidha, aliiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kukutana na benki na taasisi za fedha mbalimbali nchini kutafuta suluhu ya kupunguza riba za mikopo wanazowatoza wakopaji ili kuwawezesha wananchi wengi Zaidi kunufaika na mikopo na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Chande alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yeye ameshusha riba ya mikopo inayokopwa na taasisi hizo hiyo hadi asilimia tatu lakini kiwango cha riba cha kuanzia asilimia tisa kwenda juu kinachotozwa na taasisi za fedha kwa wakopaji bado ni kikubwa kwa wananchi wa kipato cha chini. 

Katika masuala ya masoko ya mitaji na dhamana, Mhe. Chande aliiagiza Mamlaka ya Soko la Dhamana na Mitaji (CMSA) kuongeza wigo wa elimu kwa umma kuhusu dhamana hizo na namna mwananchi anavyoweza kunufaika kwa kuwa uelewa bado ni mdogo.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja ambaye ndiye mratibu wa maadhimisho hayo alisema maadhimisho hayo hayatoi elimu pekee bali pia ni fursa adhimu kwa ajili ya kuchukua maoni na ushauri wa wananchi kuhusu maeneo mbalimbali ya huduma za fedha yanayotakiwa kuboreshwa.

Alisema maoni yaliyotolewa yamechukuliwa na yatafanyiwa kazi katika masuala ya kisera, taratibu na kutekelezaji ili kuhakikisha Sekta ya Fedha inakua na kufikia lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanafikiwa na elimu ya fedha ifikapo 2025.

Dkt. Mwamwaja alisema kuwa elimu iliyotolewa itawasaidia wananchi kufanya maamuzi mbalimbali ya kifedha ikiwemo usimamizi wa fedha binafsi, fursa za kukopa pamoja na kuainisha malengo ya kukopa, umuhimu wa kuweka akiba, usimamizi na ulipaji wa madeni, umuhimu wa bima pamoja na masuala ya uwekezaji.

Aliendelea kuwahamasisha wananchi kuendelea kushiri maadhimisho hayo ambayo yanatarajiwa kufungwa Novemba 26, 2022.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (kushoto) akisikiliza maelezo ya mifumo mbalimbali ya kifedha kutoka kwa Afisa Tehama kutoka Wizara hiyo, Bi. Stella Nguma, katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yanayoendelea katika Viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza. Katikati ni Msimamizi Mkuu wa Fedha kutoka Wizara hiyo, Bw. Salim Kimaro.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, akipokea zawadi za vitabu na machapisho mbalimbali kutoka kwa maafisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA), alipotembelea banda la Taasisi hiyo katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yanayoendelea katika Viwanja vya Rock City Mall, jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, akisikiliza maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Benki ya Biashara ya Akiba kutoka kwa Afisa Masoko wa Benki hiyo, Bw. Antony Kunambi, alipotembelea banda la benki hiyo katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yanayoendelea katika Viwanja vya Rock City Mall, jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (kulia), akizungumza na Meneja Biashara Tigo Pesa, Bi. Rastituta Kadmond alipotembelea banda la Kampuni ya Tigo katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yanayoendelea katika Viwanja vya Rock City Mall, jijini Mwanza, katikakati ni Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango, Mwanza)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.