Habari za Punde

Sekta isiyo rasmi yaongoza kwa kutoa fursa nyingi za ajira

 Na Maulid Yussuf WMJJWW. 


KAMPALA, UGANDA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amesema Sekta isiyo rasmi inaongoza kwa kutoa fursa nyingi za ajira kwa watu wanaoajiriwa au kujiajiri wenyewe.

Mhe Riziki ameyasema hayo wakati akitoa salamu za Tanzania, katika siku maalumu ya Tanzania kwenye maonesho ya 22 ya nguvu kazi/Jua kali, juu ya wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati yakiyofanyika katika viwanja vya Jamuhuri KOLOLO Kampala, Uganda.

Amesema sekta hiyo isiyo rasmi ina mchango mkubwa katika uchumi kwani bidhaa zinazozalishwa zinatumiwa na wananchi wengi na nyengine kutumika kama malighafi na wazalishaji wakubwa kwenye sekta iliyo rasmi.

Amesema Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zilikubaliana kuwepo kwa maonesho hayo kutokana na kutambua mchango wa wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati hasa waliopo katika sekta isiyo rasmi katika maendeleo ya nchi hizo.

Amesema kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni muhimu sana kwa wanachama wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani umewataka kujitambua kwa kutumia bidhaa zao wanazozalisha katika jumuiya yao.

Hivyo amewataka kutafakari juu ya bidhaa wanazozalisha kuwa ni za kutosha na zenye ubora kwa kuweza kushindana ndani na nje ya Afrika mashariki, pamoja na kutathmini bidhaa hizo kuwa na mahitaji kwa watumiaji wa Afrika Mashariki au nje ya Jumuiya hiyo.

Aidha amefahamisha kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuweka misingi ya kukuza uwezo wa nchi hizo pamoja na wananchi wake kujiletea Maendeleo kwa pamoja badala ya kutegemea uwezo mdogo wa nchi moja moja.

Amesema Serikali za Jumuiya hiyo zinahakikisha kuwa maonesho hayo yanafanyika kwa lengo la kuwapatia fursa wajasiriamali wa sekta hiyo ili waweze kutambua fursa zilizopo katika nchi wanachama na kuweza kushiriki katika uzalishaji na maendeleo ya nchi zao.

Mhe Riziki ameelezea kufurahishwa kwake kwa kuona bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali na kusema kuwa wananchi wengi wa jumuiya ya Afrika mashariki ni wabunifu na wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi kama watapewa fursa ya kufanya hivyo.

Pia amewapongeza wajasiriamali hao kwa kuzalisha bidhaa hizo na nzuri ba kuwashauri kuendelea kuwa wabunifu zaidi kwa kuzingatia kuwa biashara ni ushindani.

Amesema pamoja na mafanikio waliyoonesha, bado Serikali zao zinatambua kuwa Sekta isiyo rasmi inakabiliwa na vikwazo na changamoto nyingi zinazodumaza maendeleo ya shughuli zao na kupelekea urasimishaji kuwa mgumu.

Hata hivyo amesema Serikali imekuwa ikitatua changamoto mbalimbali zikiwemo kutoa mikopo yenye masharti nafuu, kuanzisha maeneo maalumu ya kufanyia buashara na kutoa elimu ya ujasiriamali.

Mhe Riziki ametumia fursa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwasafirisha bure wajasiriamali wa Tanzania  pamoja na mizigo yao ili  waweze kushiriki katika maonesho hayo, pamoja na kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kumruhusu nae kushiriki katika maonesho hayo.

Sambamba na hayo mhe Riziki amemshukuru Balozi wa Tanzania nchini Uganda kwa ukarimu na mapokezi mazuri pamojq na kuwashukuru waandaaji wa maonesho hayo ambapo amewaomba kuendeleza mashirikiano kati ya nchi hizo.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Uganda, balozi Dr. Aziz Ponary Mlima ameiomba Jumuiya ya Afrika Mashariki kuyaendeleza maonesho hayo kwani yanaonekana kuwa na tija kwa wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati kwa kuweza kujifunza pamoja na kutangaza biashara zao kwa kupata fursa za masoko mbalimbali.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhandisi Steven Mlote ameshauri nchi wanachama wote wa Jumuiya hiyo kuwa na sauti moja wanapofanya masuala yao ya maendeleo na kuitolea mfano Tanzania kwa kuwa na makabila tofauti lakini wameweza kufanya siku hiyo ya Tanzania kuwa ni kama kabila moja.

Maonesho ya 22 ya wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka huu  yamefanyika Kampala Uganda, ambapo jumla ya Wajasiriamali 1,500 kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo wameshiriki,  ambapo hali hiyo inaonekana kuongezeka ukilonganisha na maonesho ya mwaka jana yakiyofanyika jijini mwanza Tanzania ambapo jumla ya washiriki 1,104 walishiriki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.