Habari za Punde

Serikali kuimarisha Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia (KIST)









Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuiimarisha Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia (KIST) ili izidi kuzalisha Wataalamu watakaoweza kuendeleza ukuaji wa Sayansi na Teknolojia Nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika Mahafali ya Nane ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Mbweni Zanzibar.

Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi hiyo katika kufanikisha ukuaji wa Teknolojia Zanzibar kwa kutoa wataalamu wengi ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeandaa Mipango madhubuti ya miradi ambayo itafanywa katika Taasisi hiyo ikwemo ujenzi wa Majengo ya Madarasa na makazi ya wanafunzi.

Aidha amesema Serikali ya Awamu ya Nane imedhamiria kuzipa kipaumbele Taasisi za Elimu katika kuziwezesha kutokana na mchango mkubwa na muhimu hasa kuzalisha wataalamu wa fani za uhandisi jambo ambalo ni msingi wa Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.

Sambamba na hayo amesema kuna mradi wa (SEBET) uliolenga kuwasaidia vijana katika kuwapa ujuzi utakaoendana na soko la ajira katika Uchumi wa Buluu mradi ambao utaimarisha na kuanzisha mafunzo ya ngazi tofauti.

"Mradi huu utaimarisha na kuanzisha mafunzo katika ngazi ya Astashahada na stashahada zifuatazo; uhandisi wa vyombo vya Baharini, uhandisi wa vipoza hewa, usarifu wa mazao ya Bahari na Matunda na mboga mboga" Amesema.

Pamoja na hayo Dkt. Mwinyi amesema mategemeo ya Serikali ni kuona Taasisi hiyo inaendelea kufanya vizuri na kuahidi kuwaandalia mazingira mazuri ya kazi.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwashukuru wahisani mbali mbali walioweza kuisaidia Taasisi ya Karume tokea kuanzishwa kwake kwa kuiwezesha kupata maendeleo ya kitaaluma ikiwemo Shirika la UNESCO ambao wamefadhili kuanzisha mafunzo ya fani zinazohusisha usarifu wa mazao ya Baharini , usarifu wa matunda na mboga mboga .

Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuishukuru Mamlaka ya Mfuko wa Elimu Tanzania (TEA) kwa kutenga Jumla ya Shilingi Milioni Mia Mbili (200,000,000/=) kwa kulifanyia matengenezo makubwa jengo la Maabara ya Sayansi na Teknolojia linalogharimu Shilingi Milioni Mia Mbili thamanini na Tisa (289,000,000/=) ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa Shilingi Milioni Thamanini na Tisa (89,000,000/=) ili kufanikisha matengenezo hayo.

 Aidha ameonesha kufarijika kwake kuona makundi ya Wahandisi wataalamu (Professional engineers) waliopitia Taasisi hiyo ambao wanataka kuisaidia izidi kupata mafanikio zaidi hatua ambayo inaonesha uzalendo wao kwa Taasisi hiyo.

Nae waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa ameeleza kuwa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia inakwenda sambamba na kasi ya Serikali kwa kuwa wabunifu kwa kuanzisha fani mbali mbali zikiwemo za kukuza Uchumi wa buluu.

Aidha ameitaka Taasisi hiyo kuanzisha Fani za kuwafunza walimu watakaofundisha fani za Uhandisi ili kurahisisha kupata wakufunzi watakaosaidia kufundisha katika Taasisi hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Zanzibar Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi ameeleza kuwa Taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha Fani za Uchumi wa Buluu ili kuunga mkono Serikali katika kukuza Uchumi wake kupitia Sekta hiyo.

Vile vile amesema Taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha Kituo cha ujasiriamali kwa lengo la kusaidia vijana kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri na kuajiriwa.

Akisoma Risala kwa niaba ya Wahitimu wa Mahafali ya Nane Hamid Issa Zakaria wamemuahidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuendelea kushirikiana katika kuendeleza Taasisi hiyo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.