Habari za Punde

Ufunguzi wa Jukwaa la Mwaka la watoaji Msaada wa Kisheria

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wasaidizi wa Sheria pamoja na Wadau mbali mbali wa Sekta ya Sheria wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la watoaji wa msaada wa kisheria lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA ) Kampasi ya Maruhubi.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman akizungumza katika Ufunguzi wa Jukwaa la Mwaka la watoaji Msaada wa Kisheria lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA ) Kampasi ya Maruhubi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF Bi Lulu Ngwanakilala akitoa Maelezo kuhusiana na jitihada mbali mbali wanazochukua katika kuwasaidia watoaji msaada wa kisheria wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la Mwaka la watoaji wa msaada wa kisheria lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA ) Kampasi ya Maruhub
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Bi Hanifa Ramadhan Said akisoma maazimio ya Jukwaa ilipita la watoaji msaada wa kisheria na namna yalivyofanikiwa  katika hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Mwaka la watoaji wa msaada wa kisheria lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA ) Kampasi ya Maruhubi.
Watoaji Msaada wa kisheria na wadau mbali mbali wa Sheria wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua Jukwaa la Mwaka la watoaji wa msaada wa kisheria lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Maruhubi


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wasaidizi wa Sheria kufanya kazi kwa uweledi kwa kusimamia Misingi ya Sheria iliyopo ili kuendelea kuisaidia jamii kupata haki zao mbali mbali.

 

Mhe. Hemed ametoa wito huo akifungua Jukwaa la Pili la Mwaka la Msaada wa Kisheria lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA kampasi ya Maruhubi Zanzibar .

 

Amesema ni vyema kwa wasaidizi hao kufanya kazi kwa uweledi na kwa kuzingatia Maadili ili kazi zao ziweze kuleta tija na kuendana na Sheria zilizopo.

 

Amesema Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi imejipanga kuhakikisha Wananchi wake wanapata haki na wanafuata Katiba ya Zanzibar pamoja na Sheria zake.

 

Aidha ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwapatia mafunzo kadri hali itakavyoruhusu na kuwataka kushiriki katika Mikutano ya kikanda na Kimataifa ili kujitangaza zaidi pamoja na kupata uzoefu.

 

Mhe. Hemed ameendelea kuwataka wasaidizi hao wa Sheria kuwa wabunifu katika kuhakikisha Taasisi zao zinakuwa na nyenzo za kujiendesha kwa kubuni miradi mbali mbali ya kimaendeleo na kupunguza kusubiri kusaidiwa.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema wasaidizi hao wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia Jamii katika kutatua Migogoro mbali mbali hasa kwa kutumia njia mbadala za usuluhishi bila kuihusisha Mahakama na kuwataka kuwa karibu na Masheha kwa kuwaelimisha Wananchi juu ya masuala ya udhalilishaji na Migogoro ya Ardhi.

 

Akigusia kauli mbiu ya Jukwaa hilo Mhe. Hemed ameeleza kuwa kauli hiyo imewafiki kutokana na umuhimu wa kutumia njia Mbadala za usuluhishi katika kutatua migogoro mbali mbali katika Jamii akieleza kuwa unaendana na moja ya malengo ya Idara  Kushajihisha njia Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro kwa Jamii. 

 

Mhe. Hemed ametumia Fursa hiyo kulipongeza Shirika la Legal Service Facility (LSF) kwa kuendelea na harakati mbali mbali za kuweza kuisaidia Jamii ya Kizanzibari na Tanzania kwa ujumla katika masuala ya utoaji Msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki kwa Wanachi hasa walio wanyonge.

 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Harun Ali Suleiman ameeleza kuwa Wasaidizi wa Huduma za Sheria wanaisaidia Serikali katika kuisaidia Jamii hasa suala la utatuzi wa migogoro.

 

Aidha ameeleza kuwa Wizara itaangalia Sheria ili kuanzishwe kwa Mfuko wa Msaada wa Kisheria pamoja na Serikali kutenga kifungu cha matumizi kwa lengo la kuwasaidia Wasaidizi hao.

 

Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa (LSF) Bi Lulu Ngwanakilala amesema Tanzania ni Nchi inayopogiwa mfano kwa Kanda ya Afrika juu ya Uwepo wa wasaidizi wa huduma za kisheria hatua hiyo inatokana mashirikiano yaliyopo baina ya Shirika hilo na Serikali zote mbili.

 

Kauli mbiu katika Jukwaa hilo inasema ‘’Uimarishaji wa huduma bora na endelevu za utoaji wa Msaada wa Kisheria"

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.