Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Amepokea Gari 51 Kutoka Ujerumani *Ni ya mradi wa msaada wa dharura kuboresha shughuli za utalii na uhifadhi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Balozi wa Ujerumani nchini, Dkt. Regine Hess (kulia) wakikagua magari 51  katika hafla ya makabidhiano ya magari chini ya mradi wa dharura kwa uhifadhi na utalii Tanzania kwenye viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Disemba 20, 2022.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Balozi wa Ujerumani nchini, Dkt. Regine Hess (kulia) wakikagua magari 51  katika hafla ya makabidhiano ya magari chini ya mradi wa dharura kwa uhifadhi na utalii Tanzania kwenye viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Disemba 20, 2022. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt Pindi Chana.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea magari 51 ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa msaada wa dharura wa uboreshaji wa shughuli za Uhifadhi wa Utalii Tanzania katika hifadhi za Taifa Serengeti, Nyerere na Pori la Akiba Selous wenye thamani ya Euro milioni 20 sawa na shilingi bilioni 56.

Mradi huo unahusisha ununuzi wa magari zaidi ya 60, ndege moja na helikopita moja kwa ajili ya kuimarisha doria, uanzishwaji wa benki za uhifadhi za jamii pamoja na kuboresha mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji 55 vinavyozunguka ya hifadhi hizo.

Mheshimiwa Majaliwa amepokea msaada huo wa magari 51 kutoka Serikali ya Ujerumani leo (Jumanne, Desemba 20, 2022) katika hafla iliyofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali ya Tanzania inathamini na kutambua uungwaji mkono na Serikali ya Ujerumani kupitia Msaada wa Dharura wa uboreshaji wa shughuli za Uhifadhi wa Utalii ambao utekelezaji wake ulisainiwa Oktoba 2021 na unatekelezwa kwa pamoja kati ya TANAPA, TAWA na shirika lisilo la Kiserikali la Frankfurt Zoological Society (FZS) kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na kueleza kuwa magari hayo yatapunguza kwa kiwango kikubwa uhaba wa vitendea kazi.

Amesema lengo la mradi huo ni kusaidia shughuli muhimu za Uhifadhi na kupunguza athari zilizosababishwa na janga la UVIKO-19 kwenye utalii na uhifadhi jambo lililosababisha kadhia kubwa sana katika mapato yatokanayo na Sekta ya Maliasili na Utalii.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Tanzania inashukuru kwa msaada wa fedha za nyongeza kiasi cha Euro milioni 15 zilizotolewa na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kukabiliana na athari za UVIKO-19. Msaada huo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa wakati wa mazungumzo baina ya nchi hizo Oktoba 2021. “Nimejulishwa na timu ya wataalamu kutoka TANAPA, TAWA na KFW kwamba mradi huu kwa sasa uko katika hatua ya maandalizi.”

Amesema ufadhili huo wa ziada utasaidia kuongeza wigo wa utekelezaji wa shughuli muhimu za uhifadhi na utalii zinazoendelea katika maeneo mengine yaliyohifadhiwa na kuchangia lengo la kuhifadhi mifumo muhimu ya ikolojia kwa manufaa ya wanadamu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema miradi hiyo siyo tu inaimarisha uhusiano uliopo kati ya Serikali hizo mbili katika kusaidia sekta mbalimbali, bali pia ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa siku zijazo kati ya Tanzania na Ujerumani kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa bioanuwai kwenye mifumo ikolojia ya maeneo ya hifadhi za Taifa.

“Nachukua fursa hii kutoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi na Wakuu wa Mashirika ya TANAPA na TAWA kuhakikisha msaada huu wa vitendea kazi unaenda kufanya kazi zilizokusudiwa za uhifadhi wa maliasili na utalii na kwamba vitendea kazi hivi vitumike na kutunzwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya matumizi ya mali za Serikali.”

Kwa upande wake, Balozi wa Ujerumani nchini, Balozi Regine Hess baada ya kukabidhi magari hayo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesema kwamba Serikali yao itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu na amefurahi kukabidhi msaada huo wa magari 51.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema utekelezaji wa mradi huo utaendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria kwenye maeneo yaliyoainishwa.

 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMANNE, DESEMBA 20, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.