Habari za Punde

Jamii yatakiwa kukutana kujadili kero zinazowakabiliMratibu TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa akifungua mkutano kamati za wananchi kutoka wilaya za Pemba ulioandaliwa na Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ).


“Haki haisubiriwi, haki inatafutwa, ni lazima wananchi wawe na uelewa wa kutosha juu ya zipi ni haki zao”- WADAU


ZANZIBAR


KATIKA kuhakikisha jamii inakuwa na uwezo wa kutambua umuhimu  wa kudai upatikanaji wa haki zao za msingi, kamati za wananchi kutoka shehia za Wilaya za Micheweni, Wete, Mkoani na Chake Chake Pemba zimeshauriwa kuendelea kuwashirikisha wananchi kujadili changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi kwa njia na wakati sahihi bila kusababisha madhara.


Ushauri huo umetolewa wakati wa mkutano na kamati za wananchi kutoka shehia za wilaya hizo kisiwani Pemba ulioandaliwa na Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa lengo la kuzijengea uwezo kamati hizo kufuatilia kero zinazokwaza haki za wanawake ambazo ziliibuliwa na wahamasishaji jamii kwenye maeneo yao.


Akizungumza katika mkutano huo ambao ni utekelezaji mradi wa kuwawezesha wanawake kwenye uongozi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway Tanzania, afisa tathimini na ufuatiliaji wa TAMWA ZNZ, Moh’d Khatib, alihimiza jamii kuwa na utamaduni wa kukutana kujadili kero zinazowakabili na kukwaza haki za wanawake ili kuzitaftia suluhu kwa pamoja.


Alisema, “lazima kamati hizi zikutane na wananchi ili wao wenyewe waseme wana changamoto gani kuliko kuwasemea, hii itasaidia kuwa na uthibitisho na ushahidi wa kutosha juu ya changamoto yoyote inayotafutiwa ufumbuzi.”

Alibainisha kupitia ushirikishwaji wa wananchi kujadili changamoto na kero zinazowakabili wanawake kupata haki zao itasaidia kukuza uelewa wa jamii kushiriki moja kwa moja kudai haki zao.


“Kupitia kamati za shehia, wananchi wote wanatakiwa wawe na uwezo wa kutambua changamoto zao na wajue kuwa ni wajibu wao kuzitaftia ufumbuzi na kudai haki zao kwa kujua nani anapaswa kuzitatua ili wachukue hatua wenyewe katika kuhakikisha wanapata haki muhimu hasa wanawake,” alifahamisha.


Aidha aliongeza kuwa Ubalozi wa Norway kwa kushirikiana na TAMWA, ZAFELA na PEGAO kupitia mradi huo unalenga kujenga jamii imara yenye uwezo wa kupaza sauti kwenye kero zinazopelekea kuwakosesha wanawake haki za msingi katika jamii.


 “Lengo kubwa la mradi huu tunataka kujenga jamii ya wananchi wenye uthubutu wa kupaza sauti juu ya changamoto zinazowakabili kwenye maeneo yao hasa wanawake ili kusaidia utatuzi wa kero hizo kwa wakati,” alisema afisa huyo.


Mapemba mkurugenzi  wa mradi huo kwa upande wa PEGAO, Hafid Abdi, alifahamisha  jamii inapaswa kutambua kwamba inao wajibu wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili ili kujenga jamii yenye kufuata misingi ya usawa wa kijinsia kwa wote katika kila eneo.


Alieleza, “wananchi wanatakiwa wajue kwamba kero zilizopo katika jamii ni zao na wanao wajibu wa kuzitaftia ufumbuzi kwa njia sahihi ili kuwepo na misingi ya upatikanaji wa haki za msingi kwa kila mmoja hasa wanawake katika nyanja zote ikiwemo kiuongozi.”


Nae Mratibu TAMWA ZNZ ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa, alisema “haki haisubiriwi, haki inatafutwa, hivyo ni lazima wananchi wawe na uelewa wa kutosha juu ya zipi ni haki zao na namna gani wanapaswa kudai haki zao kwa njia iliyo sahihi.”


Mapema Mohamed Abdalla mjumbe wa kamati hizo alihimiza jamii kutumia vyombo vya habari kupaza sauti zao ili changamoto zinazowakabili ziweze kuwafikia walengwa kwa wakati.


Alibainisha, “ili changamoto hizi ziweze kutatuliwa, ni lazima sisi wananchi katika kila maeneo ambayo tunaona ni kikwazo kwetu tupate wandishi wa habari ambao watatusaidia kupasa sauti zetu.”


Kamati za wananchi katika shehia zilizoundwa kupitia mradi huo kupitia Ubalozi wa Norway zinafanya kazi kwa kuwashirikisha wananchi kujadili changamoto na vikwazo vinavyowakabili hasa wanawake na kupelekea kushindwa kupata haki zao za msingi ikiwemo ushiriki wao katika uongozi. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.