Habari za Punde

Maeneo ya Urithi wa Ukombozi Kukarabatiwa Kuvutia Utalii

 
Na Shamimu Nyaki

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amezindua Mpango wa kuweka Alama za Utambuzi katika Maeneo ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika hapa nchini, na kusisitiza kuwa lengo ni kuyalinda na kuyatangaza maeneo hayo ambayo yamebeba Historia ya Bara la Afrika.

Akizungumza Januari 17,2023 wilayani Kongwa Dodoma, baada ya kufanya ziara katika eneo hilo, ambalo ndio Kambi ya kwanza  ya Wapigania Uhuru wa Afrika,  Mhe. Gekul amesema kuwa, Tanzania imekua mstari wa mbele katika kusaidia nchi nyingine kujikomboa kwa kutoa maeneo ya kujifunzia mbinu za ukombozi, pamoja na kutoa makazi kwa wapigania Uhuru wa Bara hilo.

"Tunakarabati maeneo haya bila kupoteza historia yake, Baba wa Taifa letu  Mwalimu Nyerere alikuwa na maono mazuri ya kusaidia wengine akiamini huwezi kuwa huru kama jirani yako bado anatawaliwa, dhana hii tunatakiwa kuienzi na kuirithisha vizazi hadi vizazi, huku tukiamini yatasaidia kukuza Utalii katika nchi yetu" amesema Mhe. Pauline.

Ameongeza kuwa, Wizara itaendelea kuongeza Bajeti katika Mradi huo, huku akisisitiza Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kushirikiana na Wizara kupitia Mradi huo kuboresha miundombinu ya eneo hilo.

Naibu Waziri Gekul, amesema kuwa ukarabati utakapokamilika katika Maeneo yote ya Wapigania Uhuru, yatakabidhiwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya shughuli za Utalii.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo,  Mhe. Remidius Emmanuel ameahidi kufanyia kazi ushauri wa Naibu Waziri, ambapo amesema kwa mwaka wa Fedha 23/24 watatenga fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara katika  eneo hilo.

Mhe. Remidius ameongeza kuwa,  maeneo hayo yatakapotumika kwa shughuli za Utalii yatasaidia kuongeza uchumi wa Wananchi wa Kongwa.

Naye Mratibu wa Programu hiyo Bw. Boniface Kadili amesema mpango huo utahusisha  Kambi zote  akizitaja baadhi ikiwemo Dakawa, Mazimbu mkoani Morogoro, Tunduru mkoani Ruvuma, Lindi na nyinginezo.

Maeneo ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika nchini yalisaidia katika harakati za kukomboa nchi ikiwemo Msumbiji, Afrika Kusini, Zambia na Namibia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.