Habari za Punde

Wajasiriamali watakiwa kuzalisha bidhaa bora - wito

 Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto amewataka wajasiriamali nchini kuendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali zitakazowasaidia kuwawezesha kuwainua kiuchumi.


Amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea vikundi mbalimbali vya wajasiriamali  wakati alipoongozana na viongozi wa Taasisi za kibinafsi kutoka nchini Canada kwa lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kupinga udhalilishaji wa kijinsia.

Bi Siti amewataka wajasiriamali kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwatafutia fursa za masoko ili kuweza kuuza bidhaa zao kwa urahisi.

Aidha amewaeleza kuwa Taasisi hizo zimefanya ziara kwa lengo la kutambua changamoto mbalimbali ambazo wanakutana nazo wajasiriamali hao ili kujua njia za kuwasaidia ikiwemo kuwapatia elimu ya biashara pamoja na kuepukana na vitendo vya udhalilishaji.

Bi Siti amezitaka Taasisi binafsi na Serikali kuimarisha mashirikiano yaliyopo ili yaweze kuwasaidia wanawake nchini.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Sacred Women Aina - bibi Nia Ayodele amewaahidi wajasiriamali hao kuaandaa programu itakayoweza kuwasaidia kuwapa fursa mbalimbali za masoko pamoja na kuwapatia elimu ya uendeshaji wa ujasiriamali.

Aidha amewataka wajasiriamali hao kutokata  tamaa na kuendelea kufanya biashara za ujasiriamali ili ziweze kuendesha maisha yao.

Mapema Mkurugenzi wa Chama cha Mafunzo mama Africa na watoto kilichopo Nungwi Bi Lucy John Mpembo amewashukuru Wizara ya Maendelo ya Jamii na Jinsia kwa ushirikiano mzuri wanaoendelea kuwapatia katika mapambano ya udhalilishaji wa kijinsia katika skuli yao.

Aidha ameiomba Wizara kuwaongezea kuwapatia huduma katika sekta ya utoaji wa elimu na uwezeshaji ili kuwajengea uwezo zaidi.

Ziara hiyo imeongozwa na  Mkurugenzi wa Wizara ya Maendeleo Jinsia na Watoto, viongozi wa Taasisi ya Baraza la wakala zinazohudumia wahamiaji la Ontorio,  pamoja na Taasisi ya kimataifa ya Sacred Women kwaajili ya kutambua changamoto zinazowakabili wajasiriamali pamoja na kupinga vitendo vya udhalilishaji nchini.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.