Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kuzilinda Ndoa Zao Ili Kupunguza Idadi ya Talaka

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka Waumini wa Dini ya Kiislamu kuzilinda Ndoa zao ili kupunguza idadi za Talaka katika Jamii.

Akiwasalimia Waumini wa Masjid Aisha Jumbi Mkoa wa Kusini Unguja alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

 

Alhajj Hemed amesema kumekuwa na ongezeko la watoto wa mtaani kulikosababishwa na utoaji wa talaka kiholela kutokana na ukosefu wa subra katika ndoa jambo ambalo linapelekea kutengana kwa wazazi wa watoto hao.

                              

Amesema kitendo cha kutengana kwa wazazi kunapelekea kuibuka kwa vitendo viovu katika jamii vikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya, wizi, udhalilishaji na kuporomoka kwa maadili katika jamii.

 

Alhajj Hemed amewasisitiza Waumini hao kusimamia na kufuata maelekezo yaliyomo katika Kitabu kitukufu cha Qur-ani pamoja na Maelekezo ya Mtume Muhammad (S.A.W) ili Zanzibar irudi katika maadili mema iliyokuwa ikisifika ulimwenguni kote.

 

Pamoja na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wazazi na walezi kuwasimamia watoto kupata elimu itakayowafaa duniani na akhera.

 

Aidha amesisitiza kuitumia Misikiti kwa kujadili namna ya kuondoa matendo waovu yanayoendelea katika Jamii ya wazanzibari.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha Amani iliyopo ili kutoa Fursa kwa Serikali kuwaletea maendeleo wananchi wake.

 

Akitoa Khutba katika Sala hiyo Ustadh Muhammad Mussa Muhammad amewakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu kuutumia vyema mwezi huu mtukufu wa Rajab kwa kutafuta radhi za Allah Mtukufu kwa kufanya matendo mema.

 

Aidha amesema ni vyema Waumini kujiandaa kwa kuupokea mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kufanya kila kinachomridhisha Allah Mtukufu.


Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

27/01/2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.