Habari za Punde

Waratibu wa Wilaya watekeleze majukumu yao dhidi ya vitendo vya Ukatili na udhalilishaji wa kijinsia

 Na Maulid Yussuf WMJJWW 


Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto  bi Siti Abbas Ali amewataka waratibu wa Wilaya kupitia shehia zao kuhakikisha wanasimamia majukumu yao ya kazi ipasavyo ili vitendo  vya Ukatili na udhalilishaji  viweze kuondoka hapa nchini.

Akizungumza katika Mkutano wa Kujitambulisha kwa waratibu wa Wilaya saba za Unguja uliofanyika katika Ukumbi wa Sebleni kwa wazee, Bi Siti amesema wananchi wengi wamepata uwelewa juu ya masuala ya Vitendo vya udhalilishaji na hivyo kupelekea vitendo hivyo kuripotiwa kwa wingi pale vinapotokezea.

Mkurugenzi Siti,  amewasisitiza kutumia lugha nzuri wakati wanapofanya kazi zao ili kupata maelezo ya kina  kwa jamii inayofanyiwa vitendo hivyo pamoja na kuwasisitiza juu ya utunzaji wa siri kwa wanaotendewa vitendo hivyo.

Amesema Wizara itaandaa mafunzo maalum ili  kuwakumbusha majukumu yao ya kazi na kuwaomba wazazi  kuwa karibu  na watoto wao katika kuwaelimisha hali za kimaisha pamoja na kuwaelimisha kuwa na tabia njema.

Hata hivyo amesema amesema ataendelea kuwathamini na kuwajali kutokana na kazi ngumu waliyonayo na kuwahidi kuwapatia  vitambulisho   maalumu ili viwasaidie katika kutambulika wakati wanapofika sehemu zao za kazi.

Nae Mkuu wa Divisheni ya Watoto ndugu Mohd Jabir Makame amewataka waratibu kutambua kuwa  jukumu lao ni kuripoti matukio yanapotokea na sio kufanya usuluhishi, kwani kazi hiyo ina watu maalumu.

Hivyo amesema wanapaswa kuzingatia mipaka yao amoja na kujenga tabia ya kutafuta ushauri na maelekezo kwa wataalamu weledi wa masuala ya watoto.

Nao baadhi ya waratibu kutoka Wilaya saba za Unguja, wamesema kumeonekana kuwepo kwa kesi nyingi zinazoripotiwa kwao zinawakandamiza wanaume peke yake, hali ambayo inaonesha wakati mwengine wanawake ndio chanzo kikubwa cha kufanya vitendo vya udhalilishaji.

Hivyo wamewashauri waratibu wenzao kuwa makini juu ya hali hiyo wakati zinaporipotiwa kesi kuzisikiliza kwa makini na kutenda haki panapostahiki.

Wamesema pamoja na mafanikio wanayoyapata lakini bado wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya kutothaminiwa, na kudai kuwa baadhi ya askari Polisi nao pia wanawadharau.

Wamekuwa wakijitolea bila ya kuwa na mshahara wowote, hivyo wamemuomba Mkurugenzi huyo kuwapenda na kuwajali waratibu hao ili wazidi kufanya kazi kwa kwa imani na upendo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.