Habari za Punde

Wizara inapambana na Kupiga Vita Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia

Na Maulid Yussuf WMJJWW Zanzibar 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amesema tokea kuanzishwa Wizara hiyo wamekuwa wakipambana kwa kupiga vita kwa nguvu zote vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. 

Mhe.Riziki ameyasema hayo wakati wa hafla ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia kilimo hai, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Msonge Shakani  Wilaya ya Magharibi B Unguja.

Amesema ili iweze kufanikiwa mapambano hayo ni lazima kushirikiana kwa pamoja kila mmoja kwa nafasi yake kwa kujitoa kusaidia mapambano hayo.

"Serikali peke yake haiwezi kufanikiwa kutokomeza vitendi hivyo, kwani Kidole kimoja hakivunji chawa,  kwa hiyo ni lazima kuungana kwa pamoja kushirikiana ili kutokomeza vitendo hivyo." Amesisitiza Mhe.Riziki. 

Amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amekuwa akichukua juhudi kubwa katika kuhakikisha anapambana na vitendo vya udhalilishaji hasa kwa kuanzisha Mahakama maalumu inayoshughulikia vitendo hivyo.

Hata hivyo amesema kumekuwa na tatizo kubwa la muhali katika kuripoti matukio hayo kwa kutokuwa tayari kutoa ushahidi wakati unapofika na kupelekea kesi kufutwa, na hata kuwaficha watendaji wa vitendo hivyo.

Amewaomba kina mama  kutokubali kuvifumbia macho vitendo hivyo na kutoa ushurikiano pale linapotokea tukio hilo ili sheria iweze kuchukua hatua.

Aidha amewapongeza wanawake kwa kujitoa na  kukubali kupatiwa mafunzo hayo ili kuweza kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na wanawake na kusaidia kuipunguzia mzigo wa suala la ajira Serikali. 

Mhe Riziki amewataka kuyatumia vyema mafunzo waliyopatiwa ili waweze kujikwamua kiuchumi na  malengo ya kutolewa mafunzo hayo yaweze kufikiwa.

Pia ameishukuru Taasisi ya Kilimo hai PPIZ, Tasisi inayoshughulikia Asasi za Kiraia katika masuala ya Miradi FCS,  pamoja na Ubalozi wa Ufaransa kwa juhudi waliyoichukua kusaidia mradi huo.

Aidha ameziomba Taasisi hizo kuendelea kuwasaidia vijana na wanawake pamoja na kuwaelimisha juu ya uandishi wa miradi ambayo italeta tija kwani itaweza kuwasaidia kutatua changamoto zao zinazowakabili.

Nae Mkurugenzi wa Taasisi  ya Kilimo hai Zanzibar PPIZ ndugu Ikram Soragha,  amesema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 40 ya wanawake kati ya umri wa miaka 15 mpaka 49 wamepitia aina moja au nyengine ya udhalilishaji katika maisha yao ikiwa asilimia 25 ni wahanga wa udhalilishaji wa kingono hasa katika maeneo ya vijijini.

Kutokana na hali hiyo wameona umuhimu wa kuja na mradi  huo wa Kuwainua Wanawake Kiuchumi kupitia kilimo hai GAPE ili kuwapatia elimu wanawake kwa kuwainua kiuchumi na kuweza kujiajiri. 

Nae Mkurugenzi wa Taasisi  ya Kilimo hai Zanzibar PPIZ ndugu Ikram Soragha amesema tafiti zinaonesha kuwa asilimia 40 ya wanawake waliochini ya  15 mpaka 19 wamedhalilishwa kwa namna mbalimbali ikiwemo asilimia 25 kudhalilishwa kingono hasa katika maeneo ya vijijini.

Kutokana na hali hiyo wameona umuhimu wa  kuwakusanya baadhi ya waathirika wa matukio hayo pamoja na kuwaunganisha na wengine kupitia mradi  huo wa Kuwainua Wanawake Kiuchumi GAPE ili kuwapatia elimu na kuweza kujiajiri. 

Akisoma Risala katika hafla hiyo mmoja wa wanufaika wa Mradi huo ndugu Khadija Khamis amesema mradi  wa Kuwainua Wanawake Kiuchumi GAPE, ni wa miaka 2, umelenga kuwafikia watu 820 lakini hadi sasa tayari umewafikia watu 558.

Amesema hadi sasa tayari  umeweza kuwanufaisha  wanawake kwa kuweza kujitambua pamoja na kutambua haki zinazowahusu katika kuondokana na vitendo mbalimbali vya udhalilishaji pamoja na kuwasaidia kuweza kujiajiri badala ya kukaa na kutegemea ajira kutoka Serikalini.

Mradi wa Kuwainua Wanawake Kiuchumi kupitia Kilimo Hai GAPE, unatekelezwa na Taasisi ya Kilimo hai Zanzibar PPIZ  pamoja na Tasisi ya inayoshughulikia Asasi za Kiraia katika masuala ya miradi FCS, kwa lengo la kuwainua  wanawake kiuchumi na kuweza kujitambua na kujiajiri chini ya Ufadhili wa Ubalozi wa Ufaransa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.