Habari za Punde

Ndg.Mbeto - Aitaka Wizara ya Kilimo Zanzibar Kukamilisha Mradi wa Umwagiliaji

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Ndg.Khamis Mbeto Khamis,akizungumza nadereva wa gari maalum la kuvunia mpunga katika bonde la Mtwango.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Ndg.Khamis Mbeto Khamis,akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mhe.Hamid Seif Said katika ziara yake ya kukagua bonde la mpunga la Kilombero.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg. Khamis Mbeto Khamis, ameitaka Wizara ya Kilimo,Umwagiliaji na Mifugo nchini kukamilisha kwa wakati mradi wa umwagiliaji maji wa zao la mpunga.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kukagua mabonde ya zao la mbunga huko Kilombero Wilaya ya Kaskazini ‘’B’’ Unguja, alisema Serikali inatumia fedha nyingi katika kuandaa miundombinu ya kilimo cha zao la mpunga lakini bado mavuno yake hayaendani na thamani ya fedha zinazotumika.

Ndg.Mbeto, alisema Wizara hiyo inatakiwa kusimamia kikamilifu uzalishaji wa zao la mpunga ili Zanzibar ijitegemee kwa chakula.

Alisema Zanzibar inatumia zaidi ya tani 11,000 za mchele kwa kila mwezi hivyo kutokana na kiwango hicho ni lazima taasisi zinazohusika na masuala ya kilimo ziongeze ubunifu katika uzalishaji wa zao hilo.

Katika maelezo yake Mbeto,alisema dhamira ya CCM kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 ni kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha na inaweka akiba japo ya miezi mitatu.

Kupitia ziara hiyo aliwataka Watendaji wa Wizara ya kilimo kuhakikisha maeneo yote yenye ardhi inayofaa kwa kilimo yanatumika ili kuzalisha vyakula vya aina mbali mbali vitakavyokidhi mahitaji ya chakula kwa Wananchi.

“Bado hatujatumia vizuri rasilimali ardhi tuliyonayo kuzalisha chakula cha kutosha, mabonde ya mpunga ya kilimo cha juu na kilimo cha umwagiliaji yapo lakini uzalishaji ni mdogo haukidhi mahitaji.

Hapa kwetu wananchi wanapenda sana chakula cha Chakula ni muhimu katika maisha ya kila siku ”,alieleza Ndg.Mbeto.

Pamoja na hayo Mbeto, alisema lengo la ziara hiyo ni kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ili kujionea mafanikio na changamoto zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka ili wananchi wawe na uhakika wa chakula.

Aidha Mbeto,alilitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuharakisha ufungaji wa Transifoma kubwa katika bonde la mpunga la Kilombero ili shughuli za umwagiliaji ziendele bila vikwazo.

Naye Waziri wa Kilimo,Maliasili na Mifugo Mhe.Shamata Shaame Khamis, alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kasi kubwa ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani katika Sekta ya Kilimo.

Shaame, alisema Wizara hiyo ipo karibu na wakulima ambao ndio wadau wake wakubwa wanaohusika katika uzalishaji wa chakula.

Alisema, serikali imewekeza katika kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanalima kilimo cha kisasa na wanapata mazao mengi.

Pamoja na hayo Shaame, aliahidi kuendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza changamoto zilizopo katika sekta ya kilimo nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo Ndg.Seif Shaaban Mwinyi, alisema awali serikali ilikuwa ikigharamia gharama za pembejeo kwa asilimia 80 na wakulima wakichangia asilimia 20 lakini kutokana na kuyumba kwa Uchumi Duniani serikali inakamua wakulima hao wakitegemee.

Alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hasa za ukosefu wa mbolea nchini bado serikali imeamua kutafuta njia mbadala ya kuzungumza na Wizara ya Kilimo ya Tanzania kuona namna ya kutatua changamoto hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid, alisema bonde la mpunga la Cheju ‘’A’’ linatumiwa na wakulima zaidi 1,800 na limekuwa likizalisha kwa wingi zao la mpunga.

Alisema wananchi wamekuwa wakijiajiri wenyewe kupitia sekta ya kilimo licha ya kukabiliwa na changamoto za kumudu gharama za kununua pembejeo.

Kwa upande wake,Mkurugnzi wa Idara ya Umwagiliaji maji Zanzibar Ndg.Haji Hamid Saleh,alisema kwa sasa wanatekeleza mradi wa umwagiliaji wa zao la mpunga unaotumia kiasi cha dola za kimarekani milioni 50.

Alieleza kwamba mradi huo umejumuisha uchimbaji wa visima 35,mabwawa 3,miundombinu ya barabara yenye urefu wa mita 36.1 ambapo matarajio ni kuvuna zaidi ya tani 17,245 za mpunga kwa Unguja na Pemba.

Alisema katika kilimo hicho cha umwagiliaji wana zaidi ya hekta 1928 zitakazolimwa mpunga na kusaidia kuongezeka kwa chakula nchini.

Hamid, alifafanua kwamba Wizara kupitia mradi huo imekuwa ikitoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kinachotumia eneo dogo la ardhi na kuzalisha chakula kingi.

 Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘’B’’ Mhe.Hamid Seif Said,alisema bonde la mpunga la Kilombero limekuwa ni mkombozi kwa wakulima wa kilimo cha mbunga.

Alisema bonde hilo lina hekta 292 na linatumiwa na wakulima 2200 wanaofanya shughuli za kilimo cha mpunga.

Alisema changamoto zinazowakabili wakulima wa eneo hilo ni pamoja na uwepo wa suala la wafugaji kuachia mifugo yao katika maeneo ya kilimo pamoja na ukosefu wa huduma ya umeme kwa ajili ya kuwasha mashine za kusambaza maji.

Naye mkulima katika bonde la Mtwango Wilaya ya Kati Unguja Ndg.Shija Makenzi, alisema wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya kusambaza maji (misingi) na bomba.

Makenzi, alisema changamoto nyingine ni bei kubwa ya pembejeo zikiwemo mbolea na ukosefu wa zana za kisasa za kuvunia mpunga.

Katibu huyo wa idara ya Itikadi na Uenezi Ndg. Mbeto alitembelea mabonde ya mpunga ya Mtwango,Cheju na Kilombero.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.