Na.Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-Zanazibar) zimesaini mkataba wa mradi kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika habari za kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mradi huo wa miezi mitatu wenye thamani ya dola za Marekani 17,000, umesainiwa kati ya Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dk. Mzuri Issa Ali na Mwakilishi Mkazi wa UNESCO Tanzania, Michael Toto, katika hafla iliyofanyika Tunguu Wilaya ya kati Unguja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mzuri alisema mradi huo utaongeza nguvu mapambano dhidi ya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto ambayo ni moja ya mikakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Alisema hii ni mara ya kwanza kwa TAMWA na UNESCO kushirikiana, hata hivyo aliahidi kutekeleza mradi huo kwa kiwango ili kukidhi matarajio ya UNESCO.
Pamoja na hayo alieleza kuwa wanamatumaini makubwa na kwamba mradi huo utafanya vizuri na kuleta tija kwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Kwa upande wake mwakilishi mkaazi wa UNESCO Tanzania Michel Toto, alisema mradi huo utalenga kuwajengea uwezo wanahabari katika kuondoa mila potovu kuhusu GBV visiwani Zanzibar.
Alipongeza mchango wa wanahabari na TAMWA kwa kujikita kuandika habari za udhalilishaji na kuahidi kwamba UNESCO itaendelea kushirikiana na TAMWA katika kukabiliana na udhalilishaji ikiwemo kupunguza mimba za umri mdogo.
Pamoja na hayo alisema mashirikiano hayo ya awali yatafungua mlango kwa mashirikiano mengine zaidi ya shirikika hilo na TAMWA-ZNZ.
No comments:
Post a Comment