SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inafungua ukurasa mpya wa maendeleo kwenye uchunguzi wa ubora wa bidhaa hapa nchini kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo alipozindua maabara
mpya nne za kisasa za taasisi ya viwango Zanzibar, ZBS Maruhubi wilaya ya Mjini
mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alisema Serikali ina nia ya
dhati ya kulinda afya na usalama wa wananchi kwa kuchukua hatua stahiki za
kupima ubora wa bidhaa mbalimbali zinazotumiwa nchini.
Dk. Mwinyi alieleza taifa linashuhudia mafanikio makubwa ya utekelezaji wa
malengo ya Serikali mara baada ya uzinduzi wa maabara nyengine nne, za Vimelea, Maabara ya Vifungashio, Nguo na
Ngozi na Maabara ya Umeme yenye vifaa vya kisasa vyenye uwezo mkubwa wa kupima
sampuli na kutoa majibu ya kuaminika kwa kutumia teknolojia za kisasa.
“Ni matumaini yetu uwezo wa maabara
hizi utaleta ufanisi wa haraka katika kupata majibu ya sampuli za bidhaa
zinazoingizwa na zinazozalishwa nchini” alieleza Dk. Mwinyi.
Akizungumzia suala la kukuza uchumi wa
nchi na kupunguza umaskini, Rais Dk. Mwinyi alisema suala hilo linakwenda
sambamba na hatua ya kuimarisha maendeleo ya viwanda na biashara, aliongeza
Serikali kupitia Baraza la Wawakilishi ilitunga Sheria ya Viwango ya Zanzibar
Na. 1 ya mwaka 2011 ambayo ilianzisha taasisi ya (ZBS) mwaka 2012 na kupewa
jukumu la kuweka viwango na kusimamia ubora wa bidhaa na huduma ikiwemo
kuhakikisha soko la Zanzibar linakuwa na bidhaa zenye ubora unaostahili.
Alisema, moja kati ya changamoto kubwa
iliyoikabili taasisi ya ZBS ni kutokuwepo kwa baadhi ya maabara zenye uwezo wa
kupima sampuli za bidhaa na kupata matokeo kwa muda muwafaka nakueleza awali ZBS ilipeleka sampuli zake kwenye
maabara za taasisi nyengine kama vile za TBS, Tanzania bara lakini sasa
Serikali imelipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo kupitia maabara hizo mpya.
Hata
hivyo, Dk. Mwinyi aliwataka watendaji wa ZBS kufanyakazi kwa bidii, ubunifu, uaminifu
na kujiamini katika kusimamia majukumu yao na kuwaeleza kwamba kazi zao ni
muhimu kwa maendeleo ya viwanda, biashara na wajasiriamali katika kuimarisha
soko la bidhaa na kukuza maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri
wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban alisema suala la viwango
ni moja ya mazingira mazuri ya biashara Zanzibar.
Alieleza Zanzibar haiwezi
kufanyabiashara kwa bidhaa zisizo na viwango na kuongeza kuimarika kwa maabara
za ZBS ni moja ya maagizo ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema Wizara imezindua mfumo wa kisasa
utakaorahisisha maombi ya leseni za biashara kupitia teknolojia ya kisasa
utakaojumuisha mamlaka 45 zinazotoa leseni na kuunganisha taasisi nyengine za
Serikali zinazotegemeana zitakazofanyakazi pamoja na kuongeza, maendeleo hayo
ni mafanikio ya miaka miwili ndani ya uongozi wa awamu ya nane ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi wa Viwango
Zanzibar, (ZBS) Yussuf Nassor Majid alisema mbali ya mafanikio makubwa
yaliyofikiwa na taasisi hiyo kwa kuzindua maabara nne za kisasa pia wanatarajia
kuwa na kituo kikubwa cha ukaguzi wa magari kitakachokuwa na uwezo wa kukagua
magari 150 kwa siku, alikitaja kuwa kuwa
chA mfano kwa Afika Mashariki na Kati pamoja na maabara ya vifaa vya
ujenzi itakayofadhiliwa na World Bank itakuwa na uwezo wa kupima vifaa vyote
vya ujenzi vikiwemo nondo, kokoto, matofali, saruji, bati na vifaa vyengine vya
ujenzi.
IDARA YA MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment