Habari za Punde

Wanawake Kuendelea na Utayari na Kujitoa katika Ushindani wa Biashara ili kujiletea maendeleo wenyewe.

Na Maulid Yussuf WMJJWW. Zanzibar.

Waziri wa Maji Nishati na Madini Mhe. Shaibu Hassan Kaduara amewataka wanawake kuendelea na utayari na kujitoa katika kuwa na ushindani wa biashara ili kujiletea maendeleo wenyewe.

Mhe Kaduara ameyasema hayo mara baada ya kuzindua maonesho ya wanawake na watoa huduma katika viwanja vya Mapinduzi Square Kosonge Mjini Unguja ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani. 

Amesema siri kubwa za wafanya biashara wakubwa nchini waliopata mafanikio,  wameanzia na ujasiriamali mdogo mdogo, hivyo ni vyema nao kuendelea ili kufikia malengo yao waliyojiwekea.

AmesemaTanzania inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ambae ni mwanamke, na ni miaka miwili tu ya uongozi wake mafanikio makubwa yamepatika katika Taifa, hivyo amesema ana imani kubwa kuwa  mwanamke anaweza kuleta Maendeleo makubwa  katika nchi.

Aidha amewataka kuendelea kushirikiana kupiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kwani vitendo hivyo  vimekuwa vikiipa taswira mbaya nchi.

Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Anna Athanas Paul amewapongeza wanawake wa Zanzibar kwa juhudi kubwa wanazozifanya kwa  kujighulisha na kazi mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

Aidha amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi kubwa za kuwainua wajasiriamali wadogo wadogo nchini.

Amesema tatizo kubwa la wajasiriamali wadogo wadogo ni kutokana na kukosa masoko na ubora wa vifungashio ambao ni miongoni mwa njia za kutafuta masoko.

Akitoa salamu za wafadhili mbalimbali,  Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Ataifa linaloshughulikia usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake UN WOMEN,  bibi Lucy Tesha amesema  kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani ni  kufanya tathmini ya wanawake juu ya Maendeleo yaliofikiwa katika uchumi endelevu katika nchi na kuona haja ya kuwainua zaidi.

Akisoma risala ya Wajasiriamali na watoa huduma, Mratibu wa Wanawake na watoto ndugu Mtumwa Ali amesema, maonesho hayo yanaenda sambamba na siku ya wanawake duniani ambayo yameleta kauli mbiu ya kujikita zaidi katika matumizi ya teknolojia ili kuleta usawa wa kijinsia.

Amesema ni ukweli kuwa bado wanawake walio wengi hasa wa vijijini hawajawa na uwezo wa kutumia eknolojia, hivyo wameiomba Serikali kuwapa mafunzo wajasiriamali hao ya matumizi ya teknolojia  ili kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia na  kufanya miamala.

Amesema ukuaji wa uchumi unachangiwa pia na wajasiriamali hivyo kupatiwa mafunzo ya teknolojia kutasaidia kukua kwa uchumi wa nchi.

Hata hivyo ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Kazi Kwa kuwapa fursa ya kushiriki kwenye maonesho hayo ambayo yatawapa fursa kutangaza biashara zao ndani na nje ya nchi.

Siku ya wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8 machi kila mwaka ulimwnguni kote, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu "wekeza ubunifu na matumizi sahihi ya teknoljia kwa usawa wa kijinsia"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.