Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Akabidhi Msaada wa Vyakula

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi msaada wa Vyakula kwa ajili ya Watendaji wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa wa Kusini Pemba

Na.Ali Muhammed

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe . Hemed Suleiman Abdulla amewataka Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba kushirikiana pamoja na kudumisha upendo baina yao ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Hemed ametoa wito huo wakati akiwasalimia wanachama wa  CCM pamoja na kutoa Iftar kwa watendaji wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba katika Ofisi za CCM Mkoa wa Kusini Pemba zilizopo Chachani  Chake chake Pemba.

Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  amesema ni wajibu wa kila kiongozi kuwasaidia  watendaji  ili kuleta ufanisi mzuri wa kazi katika kukijenga Chama hicho.

Amesema ameamua kutoa mchele kilo ishirini na tano (25) kwa kila mtendaji wa Chama na Jumuiya zake  Katika mkoa huo  kwa lengo la  kuwasaidia watendaji wa Chama cha Mapinduzi waweze kufanya kazi kwa ufanisi mzuri na kutimiza malengo waliojiwekea.

Aidha Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuacha majungu, fitna na makundi yasiokuwa na tija kwa mustakabali wa  Chama na Taifa kwa ujumla.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewapongeza Viongozi waliochaguliwa katika chaguzi zilizofanyika katika  ngazi ya shina hadi Taifa na kuwataka kuwa na mashirikiano na wanaowaongoza ili kuweza kufikia shabaha ya Chama Cha Mapinduzi na kusema kuwa safu imetia kazi iendelee.

Akitoa shukrani  Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba  Ndg YUSSUF ALI JUMA amemshukuru Mhe. Hemed kwa uamuzi  wake wa kuwasaidia watendaji wa CCM katika mkoa huo na  kueleza kuwa kufanya hivyo kutaleta ufanisi mzuri wa kazi kwa watendaji na kusisitiza kuwa  kitendo hicho kina thibitisha uwezo wake wa kuongoza kwa vitendo.

Aidha ameahidi kuwa watasimamia miongozo yote yanayotolewa na viongozi wakuu kwa lengo la kukisaidia Chama Cha Mapinduzi kiweza kuendelea kushika hatamu siku hadi siku.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.