Habari za Punde

Mhe. Riziki Amewataka Wadau wa Maendeleo Kushirikiana na NGO's

Na.Maulid Yussuf. 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amewaomba wadau  wa maendeleo kushirikiana na NGOs katika kuhakikisha wanamuinua mwanamke katika nyanja mbalimbali ili kuondokana na vitendo vya udhalilishaji nchini.

Mhe Riziki ameyasema hayo katika mkutano wa pamoja wa kujadili maendeleo na changamoto zilizopo katika kumuinua mwanamke kwa kuondokana na  utegemezi pamoja na udhalilishaji, mkutano ulioambatana na ftari ya pamoja, iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake UN WOMEN kwa upande wa Zanzibar, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Madinat Al bahr Mazizini Unguja.

Mhe Riziki amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua changamoto zinazowakabili wanawake na hivyo jitihada mbalimbali zimefanyika ikiwemo kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia mikopo nafuu ili wapate fursa ya kujitafutia mitaji kuweza kufanya biashara ili kujikwamua na maisha.

Amesema pia kumeonekana upatikanaji wa mikopo hiyo kwa wanawake bado ni changamoto, amewaomba wadau hao kushirikiana kwa kuwasaidia ili kuona fursa hiyo ya mikopo wanaipata.

Kuhusu kesi za udhalilishaji kwa watoto mhe Riziki amesema tayari Wizara imeshafanya marekebisho ya Sheria ya mtoto ili kuhakikisha matukio ya udhalilishaii kwa watoto yanapungua.

Hata hivyo amelishukuru Shirika la UN WOMEN kwa kuona haja ya kuwaweka pamoja wadau hao kujadili masuala ya wanawake pamoja na kuwaftarisha jambo ambalo limezidisha upendo kati yao.

Akizungumzia masuala ya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu Zanzibar, Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman amesema kumeibuka mtindo wa kuingizwa watu wenye ulemavu nchini na  kuwatumikisha kazi ya ombamba jambo ambalo linaitia doa nchi.

" Udhalilishaji upo wa ina nyingi sio kulawiti au kubakwa tu, bali hata utumikishwaji kwa  watu wenye ulemavu nao huu pia ni udhalilishaji, ni vizuri wananchi wakautambua na  udhalilishaji huu" amesisitiza Mhe Harusi. 

Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Anna Athanas Paul amesema Wizara imekuwa ikishirikiana na NGOs na Taasisi mbalimbali katika kupiga vita vitendo vya Udhalilishaji, ili kuliweka Taifa kuwa katika mazingira mazuri na Salama.

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake UN WOMEN,  kwa upande wa Zanzibar bibi Lucy Tesha amesema madhumuni ya Mkutano huo ni kujadiliana mafanikio na changamoto katika  ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, maendeleo yaliofikiwa katika kumuinua mwanamke kiuchumi Zanzibar pamoja na kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa pamoja katika kuleta maendeleo kwa wanawake.

Kwa upande wao washiriki wa Mkutano huo wamesema bado kuna kuna ushirikishwaji mdogo katika kuwainua wanawake katika nafasi mbalimbli za uogozi, wajasiriamali kutojiamini na kutotumia mitandao ya kijamii katika kutafuta masoko.

Hata hivyo wamesema katika suala la udhalilishaji hawapo tayari kuona mtoto wa kike nae anafungwa katika kesi za miaka 14 mpaka 18, kwani hiyo ni kuendelea kumkandamiza mwanamke.

Mwisho
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.