Mwenyekiti wa Taasisi ya Majlis Al-Maarif Islamiya Tahir Khatib Tahir alipokua akitoa mkono wa Iddi kwa watoto waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja wakati Taasisi hiyo ilipofika kuwafariji Wagonjwa hospitalini hapo.April 22,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Na.Fauzia Mussa - Maelezo Zanzibar
Wazazi wenye Watoto wanaosumbuliwa na maradhi makubwa ikiwemo saratani wamewaomba Viongozi wa Serikali ,Taasisi binafsi na watu wenye uwezo kujitokeza kusaidia gharama za matibabu ili watoto wao waweze kupona kwa haraka na kujumuika na watoto wenzao katika mambo mbalimbali ikwemo kusherehekea skukuu ya Iddi.
wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa mkono wa Iddi kutoka kwa Taasisi ya Majlis Al-Maarifa Islamia wamesema watoto wao wamekua wakiugua kwa muda mrefu sasa na hali zao zimeshindwa kutengamaa kutokana na kutokumudu gharama za matibabu kwa watoto hao.
walieleza kuwa kutokana na magonjwa wanayougua watoto wao wanahitaji kuwa na Bima za Afya ili kupata matibabu kwa wakati sahihi hivyo wameziomba taasisi na wenye uwezo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kurudisha Afya za watoto wao.
"mtoto alianza kuumwa tangu ana miezi saba hadi sasa ana miaka mitatu na miezi, alianza uvimbe katika shingo unaojirudia mara kwa mara tukawa tunakuja na kurudi spitali baada ya kuhangaika kwa muda mrefu ndio ikagundulikana mwanangu anasumbuliwa na saratani katika shingo na tumbo kujaa maji"alielezea mama Azida
"hali zetu za kimaisha ni duni hatuna uwezo wa kufanya vipimo wala kutibiwa spitali binafsi inabidi tu tusubiri mkono wa Serikali na rehma za mungu "alieleza mmoja wa wazee hao.
Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya Majlis Al-Maarif Islamiya Tahir Khatib Tahir amesema mbali na kufika Hospitalini hapo kuwafariji Wagonjwa kwa kuwapatia mkono wa Iddi vilevile ziara yao hiyo ilikua na lengo la kuwatafuta watoto wenye kesi maalum na kuweza kuwasaidia katika matibabu.
Alieleza kuwa Taasisi hio ina mpango wa kuwasaidia watoto kumi wenye maradhi sugu na kesi maalum kwa kuwapatia bima ya Afya ya NHIF ili kuisaidia Serikali kurahisisha harakati za kurejesha Afya zao.
Aidha alifahamisha kuwa watoto mayatima na wenye mazingira magumu wanawapa kipaombele katika mpango wao huo unaekwenda kuzifariji familia za watoto hao wanaosumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu bila ya kujali dini.
"licha ya kuwa Taasisi yetu ni ya Kiislamu lakini hatusaidii kwa kipengele cha Dini kwani furaha ya kila mmoja ni uzima tupo tayari kuwasaidia watu wote kadiri hali inavyoruhusu bila kujali Dini,rangi wala kabila sharti awe amaekidhi vigezo tu".Alifahamisha Mwenyekiti huyo.
Kwaupande wake Daktari dhamana msaidizi Jengo la Mnazimmoja Fatma Khamis ameishukuru Taasisi ya Majlisi Al-Maarif kwa hatua walizozichukua za kuwapatia Bima ya Afya kwa wale wenye mahitaji maalum mara baada ya kuwagundua walipofika Hospitalini hapo kwa ajili kuwafariji katika kipindi hichi cha Skukuuu .
Vilevile Dkt,Fatma amezikaribisha Taasisi Binafsi na watu wenye uwezo kutembelea Hospitalini hapo kuangalia Wagonjwa na kuweza kuwasaidia kwani baadhi yao wana matatizo makubwa na uwezo wao ni mdogo.
" kuwajali na kuwahurumia Wagonjwa ni miongoni mwa ibada zinazompendeza mungu,hivyo ni vyema tukiwa karibu nao ili kujivunia thawabu katika muda wote na sio kipindi hichi tu cha skukuu "alishauri Dkt. Fatma .
Takribani Watoto mia moja katika hospitali ya Mnazimmoja wamenufaika na mkono wa Iddi kutoka kwa Taasisi ya kijamii Majlis Al- Maarif Islamia.
No comments:
Post a Comment