Habari za Punde

Alhajj Mwinyi -Amewahimiza Wawekezaji Kuangalia Changamoto za Jamii na Kuona Haja ya Kuwasaidia katika Kuzitatua.

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza wawekezaji kuangalia changamoto za jamii na kuona haja ya kuwasaidia katika kuzitatua.

Al - hajj  Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa msikiti wa masjid Al – Marhoum Abdel Moeim Shahein, uliopo Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Al - hajj  Rais Mwinyi,  alisema mara nyingi Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar inawashajihisha wawekezaji wanaokuja Zanzibar kufanya biashara zao, waone umuhimu wa kushirikiana na jamii zilizowazunguruka kwenye shughuli za biashara zao ili kuwasaidia katika mambo mbalimbali ikiwemo kuwajengea misikiti, huwasaidia kupata huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na maji safi.

“Tunawataka wawekezaji waone umuhimu wa kuzisadia jamii kule wanakoekeza biashara zao, wawekezaji wanaweza kusaidia kama hivi ujenzi wa misikiti na madrasa au kwenye huduma za jamii ikiwemo kuwasaidia kuwafikishia jamii, maji safi na salama, elimu au afya.” Alieleza Al hajj Dk. Mwinyi.

Al - hajj  Dk. Mwinyi, aliwasisitiza wawewkezaji kuhakikisha jamii zinazowazunguka kwenye uwekezaji wao, wanazisaidiana kwa hali na mali.

Aidha, aliwasisitiza waumini wa msikiti huo mbali ya kutekeleza ibada za sala lakini kuanshisha kituo cha kuhifadhia Quran kwa vijana wa Zanzibar ili kuendelea kukitukuza na kukienzi kitabu kitukufu cha Quran.

Pia Al - hajj  Dk. Mwinyi, alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshururu mfadhili wa msikiti huo kwa kuisadia jamii ya watu wa Kizimkazi.

Akizungumza kwenye ibada hiyo ya sala ya Ijumaa, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume alitoa wito kwa wahisani na wafadhili wa ndani na nje, kuangalia uwezekano wa kuzisaidia jamii kwa kuwajengea zenye hadhi nzuri kama ilivyo kwa ujenzi wa misikiti mingi mikubwa na ya kisasa.

Alisema, madrsa nyingi za Zanzibar hazipo kwenye hali nzuri katika ustawi wa kuwafundisha mema wanafunzi.

Alizungumzia baadhi ya changamoto zinazozikumba madrasa nyingi za Unguja na Pemba, Katibu Khalid alieleza kuna baadhi ya madrasa hazina vyoo, ufinyu wa nafasi kwa kuwa na vyumba vidogo vya madarasa kwa wanafunzi wanaume na wanawake.

Mapema, akisoma risala ya ufunguzi wa msikiti huo, Ustadhi Mahfoudh Said Omar alieleza historia ya msikiti huo awali ilikua shamba walilolinunua kukoka kwa mmoja wa wanakijiji wa Kizimkazi Mkunguni, ambapo walianzia na msikiti wa miti mwaka 2001 ambao uliendelea kutekelezewa ibada hadi mwaka mwaka 2022 alipotokea mfadhili sheikh Sharif Abdel Shahein kutoka Misri na kuwajengea msikiti huo wa kisasa na Madrasa yake.

Kwa upande wa waumini kijijini hapo waliahidi kuutunza vyema msikiti na madrsa hiyo kwa mujibu wa miongozo kutoka ofisi ya mufti ili kuakisi dhima halisi ya jenzi wa msikiti huo kwa kuwaandaa vijana kijijini hapo na vijiji jirani kuwahifadhisha kitabu cha Mwenyezi Mungu (S.W) Qurani tukufu.

Walieleza lengo la ujenzi wa msikiti huo ni kuendeleza kufanya ibada na kutoa vijana wenye maadili mema na kutunza jamii iliyo bora.

Ujenzi wa msikiti wa masjid Al – Marhoum Abdel Moeim Shahein wa Kizimkazi, umefadhiliwa na sheikh Sharif Abdel Shahein wa Misri ambae alieleza dhamira yake ya kumuenzi mzee wake, Al – Marhoum Abdel Moeim Shahein aliefariki miaka miwili iliyopita.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.