Habari za Punde

Waziri Pembe Atowa Mkono wa Pole kwa Familia ya Marehemu Bi.Kidawa

Na.Maulid Yussuf -Zanzibar  WMJJWW.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar imetoa pole kwa familia ya Marehemu Bi.Kidawa kufuatia kifo chake na mtoto wake kilichosababishwa na uzembe wa baadhi ya wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja  Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar juzi. 

Akitoa pole hiyo  huko Dimani Waziri wa Wizara hiyo Mhe Riziki Pembe Juma amesema Wizara ipo pamoja na familia hiyo  kutokana na msiba huo na kuwaomba kuwa na subira kutokana kipindi kigumu walichokuwanacho.

Aidha Mhe Riziki ameiomba Wizara ya Afya kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio la vifo hivyo vya mama na Mtoto wake na atakaebainika kuhusika hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa haraka.

Amesema Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amekuwa akifanya jitihada mbalimbali katika kuimarisha huduma za afya kwa  kujenga Hospitali kubwa za kisasa pamoja na vifaa, kuongeza mishahara kwa wafanyakazi, kwa lengo la kuweka mazingira mazuri kwa wananchi  na wafanyakazi wake.

Amesema kuna baadhi ya watu wachache wamekuwa wakiharibu kwa makusudi juhudi  hizo, hivyo ni vyema wakachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe ni fundisho kwao na kwa wengine.

"Kweli tunakubali kifo kimeumbwa, lakini kwa hili naamini Serikali haijaenda Iikizo, na haitawavumilia wote  waliohusika na uzembe  kama huu," amesisitiza Mhe Riziki 

Nae Mume  wa marehemu ndugu Nassor Omar Waziri amesema ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kufika kuifariji familia hiyo, na kusema kuwa ana imani na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutenda haki kwa wananchi wake.

Marehemu mwalimu Kidawa  Khamis Haji, alikuwa mwalimu wa Skuli ya Msingi  Kidongochekundu amefariki Mei 15 majira ya saa tano asubuhi,
Mungu amlaze Mahali pema Peponi Amin.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.