Habari za Punde

Wizara ya Ardhi Kutoa Hakimiliki za Kimila 520,000 mwaka 2023/24

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2023/24 imejipanga kuandaa na kutoa Hati za Hakimiliki za Kimila 520,000, Hatimiliki 500,000, Hati za Sehemu ya Jengo 1,000 na itasajili Miamala ya Hatimiliki na Nyaraka za Kisheria 100,000.

Taarifa hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma wakati Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Dkt. Angeline Mabula akiwasilisha ohtuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24.

Waziri Dkt. Mabula alisema kuwa, Wizara haikuweza kufikia malengo katika uandaaji na usajili wa Hatimiliki na Hati za Hakimiliki za Kimila kutokana na kuchelewa kuanza kwa Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi, kutokamilika kwa wakati miradi ya KKK katika mamlaka za upangaji, wananchi wengi kutokamilisha ulipaji wa gharama za umilikishaji na changamoto ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Alifafanua kuwa, hadi kufikia Mei 15, 2023, Wizara imeandaa na kusajili Hatimiliki 76,746, imetoa Hati za Hakimiliki za Kimila 51,762, imeandaa vyeti vya Ardhi ya Kijiji 67, imesajili Hati za Sehemu ya Jengo 300, Miamala ya Hatimiliki na Nyaraka za Kisheria 92,124 pamoja Hatimiliki na Nyaraka za kisheria 100,000.

"Kwa mwaka huu wa fedha, Wizara inatarajia kufanikisha malengo hayo kwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Milki za Ardhi, Programu ya Kupanga, Kupima na kumilikisha Ardhi (KKK), na Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Upimaji na Ramani kwa kushirikisha wadau wa sekta binafsi, kuimarisha mifumo ya TEHAMA ambayo itarahisisha utoaji wa Hatimilki na kupitia upya viwango vya tozo na ada za umilikishaji ili kuleta unafuu kwa wananchi", amesema Waziri Mabula.

Ameongeza kuwa, Wizara imeendelea kuandaa na kusajili Hatimiliki na Hati za Hakimiliki za Kimila kwa wananchi na taasisi na kutoa Vyeti vya Kijiji ambapo umuhimu wa Hatimiliki hizo ni kuongeza usalama wa milki na kuwezesha kupunguza migogoro ya ardhi. Vilevile, Hatimiliki hizo zinaweza kutumika kama dhamana kwenye Taasisi za Fedha na vyombo vya kisheria

Aidha, amewahakikishia wananchi na taasisi za fedha kuwa Hati za Hakimiliki za Kimila ni nyaraka halali za kisheria hivyo, amesisitiza waendelee kuzitumia kwa manufaa ya kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.