Na.Luluwa Salum. OMPR.
Makamu wa Pili wa Raisi wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewaagiza wakandarasi na washauri elekezi kuhakikisha wanasimamia viwango na ubora wa masoko yanayojengwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akitembelea ujenzi wa miradi hio Mhe. Hemed ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa masoko hayo yanatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.
Amesema kumaliza kwa masoko hayo kutatatua kero ya wananchi na wafanyabiashara ambao kwa sasa wanafanya biashara zao mazingira yasiyo rasmi hali ambayo inachangia kupotea kwa mapato ya Serikali.
Aidha Mh Hemedi amewaagiza wakandarasi wa masoko hayo ambao ni Jeshi la kujenga Uchumi, Chuo cha Mafunzo na Kikosi cha zima moto na uokozi kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa ufanisi mkubwa na kuahidi kuyatembelea kila baada ya mwezi ili kufuatilia maendeleo ya ujenzi huo.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuamua kuvikabidhi Vikosi vya SMZ kujenga masoko hayo jambo ambalo limeipunguzia gharama Serikali ya kuajiri wakandarasi kutoka nje.
Aidha ameridhishwa na utendaji kazi wa Uongozi wa Mamlaka ya usajili wa Majengo (ZBA) kwa kusimamia viwango na ubora wa majengo hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi itaendelea na ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo bila ya kusita na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu kipindi chote cha ujenzi wa miradi hiyo.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Muhamed amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Wizara itasimamia na kufuatilia kwa karibi ujenzi huo ili kufikia azma ya Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuwawekea mazingira mazuri wafanyabishara yanafanikiwa.
Nae Katibu wa Idara ya Siasa, Itikadi na uenezi Khamis Mbeto Khamis ameeleza kuwa Ibara ya 238 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwenye kifungu cha serikali za mitaa imeelekeza serikali kuhakikisha ianweka mazingira bora kwenye halmashauri kuanzia masoko na maeneo mengine kwa ajili ya wananchi.
Kwa upande wao wakandarasi na washauri elekezi wa ujenzi wa masoko hayo wamesema licha ya changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza wamemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa masoko hayo yatamalizika kwa wakati uliopangwa na kwa ubora mkubwa.
Ziara hiyo imejumuisha ujenzi wa soko la Mwanakwerekwe, soko la Jumbi na Soko la Chuini ambapo kumalizika kwa masoko hayo yatanufaisha zaidi ya wafanyabiashara Elfu Tisa Mia Tano (9,500) sambamba na kuongezeka mapato ya Nchini.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
01/06/2023
No comments:
Post a Comment