Habari za Punde

Mhe Hemed mgeni rasmi katika maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu 1445

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na  Mufti Mkuu wa Zanzibar Samahatu Sheikh Saleh Omar Kaabi wakti alipowasili katika Masjid Jamiu Zinjibari kuhudhuria  maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu 1445
  

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewaongoza waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla katika shamrashamra za maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislam 1445-Hijri pamoja na Dua maalum ya kuiombea Nchi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Masjid Jamiu Zinjibar.

 

Viongozi mbali mbali wamehudhuria katika Dua hiyo akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Samahatu Sheikh Saleh Omar Kaabi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Harun Ali Suleiman, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu, Viongozi wa Dini na Serikali wa ndani na nje ya Zanzibar , na waumini wa Dini ya Kiislamu. 

 

Akitoa Nasaha katika Dua hiyo Sheikh Sameer Zulfikar Ramzan Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar ameeleza kuwa Hijra ya Mtume Muhammad (S.A.W) ya kuhama Makkah na kuhamia Madinah imepelekea mabadiliko makubwa katika Mji wa Madinah ikiwemo mfumo wa uendeshaji wa biashara, kuimarika Uchumi na mbinu za ufugaji na kilimo jambo ambalo tunapaswa kuliiga kwa ustawi wa uchumi na maendeleo kwa wazanzibari.

 

Aidha amewaasa waumini hao kuzingatia miongozo ya Qur-ani na hadithi za Mtume (S,A,W) katika maisha ya kila siku.

                       

Nae Shekh Khamis Gharib kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ameeleza kuwa ni wajibu wa waumini kuwa na muamko wa kujitolea kuendesha harakati za Kiislamu, na kusisitiza kutumia vyema mali za wakfu kama Uislamu ulivyoeleza.

 

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amewashukuru waumini waliojitokeza kwa wingi na wale wote waliofanikisha shamrashamra za maadhimisho hayo.

 

Aidha amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuridhia kuwa kila ifikapo Mwezi mosi Muharram  ya kila mwaka kuwa ni siku ya mapumziko ya kitaifa.

 


Maadhimisho ya mwaka Mpya wa Kiislamu 1445 - Hijria mwaka huu ni Maadhimisho ya kwanza kufanyika Kitaifa baada ya Kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuridhia siku ya mwaka mpya wa Kiislamu kuwa ni mapumziko.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.