Habari za Punde

Jamii Yatakiwa Kusimamia Watoto Kwenye Malezi Mema Ili Kupata Taifa Bora - Alhajj Hemed

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ameitaka Jamii kusimamia watoto kwenye Malezi mema ili kupata Taifa bora lenye vijana wazalendo na wenye uchu wa maendeleo ya Zanzibar.

Alhajj Hemed ameeleza hayo wakati akiwasalimia waumini wa Masjid Islah Chakechake Pemba alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

 

Amesema Zanzibar ni nchi yenye historia nzuri kwa wananchi wake kuwa na Tabia, silka na tamaduni njema zilizofanya kuitangaza Zanzibar Kitaifa na Kimataifa hivyo, Wazazi na Walezi ni vyema kusimamia dhima hiyo ili kupata jamii iliyosalimika na vitendo viovu.

 

Alhajj Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali inaendelea kuweka mikakati Mizuri ya kielimu kuanzia elimu ya Maandalizi, msingi, Sekondari hadi Chuo ili vijana waweze kupata elimu  ya lazima kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wazazi na Walezi kuwashauri vijana wao wanaomaliza elimu ya Sekondari kufanya maamuzi sahihi wanapochagua masomo yao elimu ya juu kwa kuzingatia Fani zilizopewa kipaumbele na Serikali ikiwemo Ualimu wa Sayansi pamoja na Madaktari Bingwa wa Magonjwa mbali mbali.

 

Aidha Alhajj Hemed ameitaka jamii kuyasaidia makundi Maalum ikiwemo watu wenye ulemavu, Mayatima, wazee na vijana jambo ambalo litaongeza mashirikiano na mapenzi katika Jamii.

 

Akitoa khutba ya Sala ya Ijumaa Shekh Walid Muhsin Juma ameikumbusha jamii ya waislamu kuwa na mapenzi baina yao na kuwa na tabia ya kustiri aibu za wengine na kueleza kuwa huo ni msingi wa kupata radhi za Allah (S.W).

 

Amesema Muumini wa kweli ni vyema kufanya mema kwa kufuata maamrisho ya Qur-an na Sunnah ili kutafuta radhi za Allah (S.W) Duniani na kesho Akhera.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.