Habari za Punde

Mhe Othman akutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Taasisi ya Mpango wa Hiari ya kujitathimini katika masuala ya Utawala Boara Afrika

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman ( kulia) akizungunza na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Mpango wa Hiari ya kujitathimini katika masuala ya Utawala Boara Afrika ( APRM), Bwana  Lamau Mpolo huko ofisini kwa Makamu Migombani mjini ZANZIBAR leo tarehe 22 Agosti 2023. ( Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar)

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman , amesema kwamba kuwepo kwa Taasisi ya Kujitathmini kwa hiari  Afrika katika masuala ya Utawala Bora ni fursa muhimu ya kusaidia kukuza uchumi na maendeleo endelevu nchini.

Mhe. Othman ameyasema hayo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Taasisi hiyo kutoka Tanzania Bara uliongozwa na Katibu Mtendaji wake Bwana Lamau Mpolo.

Mhe. Othman amesema kwamba taasisi hiyo inapaswa kuelekeza juhudi zake kwa  kuangalia kasoro na mapungufu  kwenye masuala mbali mbali  katika kuchangia kasi ya uwajibikaji ili kuimarisha uchumi na kuiwezesha nchi kuondoka mahali ilipo sasa na kuweza kusonga mbele kimaendeleo.

Amefahamisha kwamba masuala yanayohusishwa na taasisi hiyo ya kujitathimini  katika suala la utawala bora yanagusa  uwajibikaji  kwa viongozi na wananchi ni muhimu hasa kwa vile yanazingatia maeneo yote ya kiuchumi na kimaendeleo kwa taifa na jamii kwa jumla .

Amesema katika kuunga mkono juhudi hizo ni lazima taasisi hiyo kupewa umuhimu stahiki kutoka kwa jamii watendaji na serikali kwa jumla ili iweze kuakisi vyema mahitaji na mipango bora ya maendeleo kwa nchi kwa kuwa masuala hayo yanamchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Amesema kwamba iwapo masuala hayo yatapewa umhimu unaostahiki inawezekana ndani ya Tanzania kuwepo matokeo chanya ya kimaendeleo kwa taifa katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi  na taifa kuweza kupiga hatua kama ilivyofanyika katika nchi mbali mbali duniani.

Aidha amesema kwamba masuala hayo yanapopewa msukumo stahiki pia yanachangia  kuimarisha mahakama zenye ufanisi mkubwa ambazo ni moja kati ya nyenzo kubwa za kiuchumi na maendeleo.

Amefahamisha kwamba nchi mbali mbali zenye mahakama zinazowajibikaji kwa ufanisi zimechangia sana mataifa hayo kuweza kupiga hatua katika kukuza uwekezaji kwenye sekta na maeneo mbali mbali  na hivyo kuimarisha upatikanaji wa mapato na kukuza uchumi wa nchi zao jambo ambalo linaweza kutumika pia kwa Tanzania na ikaweza kupiga hatua.

Aidha Mhe. Othman amesema kwamba iwapo masuala hayo  yatasimamiwa ipasavyo yatasaidia sana katika kurejesha imani kwa wananchi  kwa kuwa viongozi pia watasiamia maadili na kuitaka taasisi hiyo kuzitangaza kwa wananchi shughulizao mbali mbali wanazofanya   ili kujenga uwelewa bora kwa umma.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Mapngo wa hiari wa kujitathimini katika masuala ya utawalabora na demokrasia Afrika nchini Tanzania Lamau Mpolo amesema kwamba Taasisi hiyo ni muhimu na inaendelea na jitihada za uratibu katika dhana ya utawala bora kwa kuonesha kasoro na kutoa mapendekezo juu ya namna ya kufanya marekebisho katika maeneo mbali mbali.

Amesema kwamba hivi karibuni taasisi hiyo itapita kwa wananchi katika maeneo mbali mbali ya Tanzania ili kusikiliza maoni hasa katika vigezo vya siasa , uchumi na utawalabora ambavyo ndivyo vinavyotumika katika tathimi wanazozifanya.

Taasisi  ya Mpango wa hiari ya kujitathmini katika masuala ya utawala bora na Demokrasia  Afrika tayari imeridhiwa na  nchi 43 kati ya 54 za Afrika yenye madhumuni ya kukuza dhana ya utawala bora kwa kuzingatia vigezo  vya ustawi wa kiuchumi kwa jamii, siasa ,  Demokrasia  ili kuleta  maendeleo endelevu.

 Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Agosti 22, 2023.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.