Mjumbe wa Kamti Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Zanzibar kupitia sekta mbalimbali bila ya kujali tofauti ya aina yoyote.
Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi, wanachama wa CCM na wananchi wa Jimbo la Chake chake alipokuwa akihitimisha ziara yake ya Majimbo Hamsini ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Amesema dhamira ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ni kuijenga Zanzibar katika nyanja zote kiuchumi, kisiasa na jamii ili wananchi wawe na mazingira mazuri yaliyo bora.
Amefahamisha kuwa Serikali itahakikisha Kiwanja cha michezo cha Tibirinzi kinajengwa cha kisasa chenye hadhi ya Kimataifa ili kuibua vipaji na kukuza michezo nchini.
Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali imeanza ujenzi wa Viwanja vya michezo vya kisasa kila Wilaya ambacho ujenzi wa Kiwanja cha Tibirinzi kitatoa fursa kwa vijana wa maeneo ya Chake chake na maeneo jirani kuweza kukitumia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema malengo ya Rais Dkt. Mwinyi ni kuufanya Mji wa Chake chake kuwa ni sura ya Kisiwa cha Pemba ambapo kukamilika kwa Bustani ya kupumzikia eneo la Mwanamashungu, ujenzi wa Barabara kutoka Chake hadi Wete pamoja na miundombinu ya Taa za Barabarani kutasaidia kuweka haiba nzuri ya mji huo.
Amesema Serikali ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi zinasogeza huduma za kijamii maeneo yote ili wananchi wote wanufaike na uwepo wa Serikali zao.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ameupongeza Uongozi wa Jimbo la Chake chake kwa mashirikiano mazuri waliyonayo baina ya Serikali na Chama na kuwataka wanachama kuungana na viongozi wao katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Sambamba na hayo amezishukuru Kamati zote za Siasa kuanzia Tawi hadi Mikoa kwa maandalizi mazuri ya ziara katika majimbo yote Hamsini hatua ambayo inaonesha utayari wa viongozi hao katika kukiimarisha Chama.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
31 Agosti, 2023
No comments:
Post a Comment