Habari za Punde

Mjumbe wa Kamati Kuu Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndg.Hemed Suleiman Aendelea na Ziara Yake Pemba Jimbo la Tumbe


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akiweka Jiwe la Msingi Tawi la CCM Shumba Viamboni akiendelea na ziara yake ya kuimarisha Chama Jimbo la Tumbe Mkoa wa Kaskazini Pemba

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Awamu ya Nane inayoongzwa na Dkt. Hussen Ali Mwinyi imejipanga kuifungua Pemba kiuchumi jambo ambalo litatanua wigo wa kibiashara Ksiwani humo.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Tumbe na Jimbo la Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba katika ziara yake ya kukiimarisha chama cha Mapinduzi katika Majimbo yote hamsini ya Uchaguzi.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ya kujenga Miradi Mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Bandari, uwanja wa ndege wa Kimataifa na miundmbinu ya barabara itafungua Pemba kiuchumi na  kuongeza kipato cha Taifa na mtu mmoja mmoja.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar italitumia eneo la Mkoa wa Kaskazini Pemba katika kukuza fursa za uwekezaji katika sekta ya Utalii na ujenzi wa Viwanda ambao utatengeneza ajira kubwa kwa Vijana wengi nchini.

Amesema mpango mkuu wa Serikali ni kuzijenga barabara zote kwa kiwango cha lami ili kusaidia uwekezaji na kurahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa.

Aidha ameeleza kuwa bandari ya shumba  imesharasimishwa na muda mfupi ujenzi wa bandari hio utaanza ambapo kumalizika kwake  kutaleta Ustawi bora kwa wananchi wa Tumbe na vijiji jirani.

Amewaahidi vijana  kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kusimamia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi kuwa vijana wawe  kipaombele zitakapotokezea fursa sambamba na Mradi wa Vijana utakaosaidia kupatiwa fedha za  uwezeshaji ili kuweza kunufaika kupitia sekta ya uwezeshaji .

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa shughuli kubwa za wakaazi wa Tumbe na maeneo jirani ni ukulima na uvuvi hivyo Serikali itawapatia vifaa vya kisasa vitakavyowasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Amewaahidi wananchi wa Tumbe kuwa Serikali itasambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo sambamba na kutatua changamoto ndogo ndogo zilizobakia katika sekta ya Elimu na Afya.

Amesisitiza kuwa Majimbo hayo yataendelea kuwa ngome ya CCM na isitokee vyama vya upinzani kuongoza Jimboni hapo hivyo amewataka viongozi na wanachama wa CCM kushirikiana pamoja katika kukiimarisha Chama kwa kuondoa makundi na mipasuko ndani ya chama ambayo  inazorotesha uimarikaji wa chama.

Amewataka viongozi kuwasimamia na kuwashawishi wanachama kujenga tabia ya kulipa ada ya Chama bila kushurutishwa  kwani ulipaji wa ada kwa wakati ndiko kunakohalilisha uanachama wao ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

Nae Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndg Hamad Hassan Chande ameeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni Chama chenye sera zinazotekelezeka na zinazolenga kuwaletea maendeleo wazanzibar.

Amewataka wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla kuwaunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa dhamra yao ya kuwaletea maendeleo watanzania.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe. Maida Hamad Abdallah ameeleza faraja ya vikundi mbali mbali kunufaika na mikopo ya uwezeshaji hasa kina mama hatua ambayo itawasaidia kuweza kujishughulisha na kuacha kuwa tegemezi kwa Familia.

Katika ziara hiyo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amepokea wanachama tisa kutoka vyama vya upinzani waliorejesha kadi za vyama vyao na kupatiwa kadi za uanachama wa CCM pamoja na kuwapatia kadi zaidi ya wanachama wapya sabini (70)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.