Habari za Punde

Ufunguzi wa Studio ya 3D Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolijia Zanzibar

 
Na.Mwandishi wa KIST.

Mkuu wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi, amesema upo umuhimu mkubwa wa kuwepo studio ya 3D katika Taasisi ya Karume ili kuwawezesha wanafunzi kuongeza ujuzi uliobora katika  masomo yao.

Amesema hayo katika hafla ya ufunguzi wa Studio ya 3D, (iliyofadhidiliwa na Taasisi ya TIKA kutoka nchini Uturuki), iliofanyika katika ukumbi wa Mkutano wa  Dkt Idrissa Muslim Hijja, Mbweni Zanzibar.

Ameeleza kuwa, kutokana na ukuaji wa teknolojia duniani, Taasisi ya Karume imeona upo umuhimu mkubwa wa kuwafundisha wanafunzi teknolojia ya 3D ili wapate ujuzi wa kisasa utakaowawezesha kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.

Aidha, Dk. Mahmoud ametumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya TIKA kutoka nchini Uturuki kwa kuonesha ushirikiano mzuri kwa Taasisi ya Karume hasa katika miradi ya Elimu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Karume, Dk. Afua khalfan Mohamed, amesema uwepo wa studio ya 3D katika Taasisi ni miongoni mwa fursa muhimu kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla,  hasa wenye uhitaji wa kufanya kazi za kisasa, hivyo ni muhimu kuitumia vizuri fursa hiyo.

Dk. Afua amesema, ni vyema kuweka mikakati mizuri ya kuifanya studio ya 3D katika Taasisi ya Karume, iwe ni miongoni mwa vituo vinavyozalisha wataalamu walio bora kwa  Zanzibar.

Nae Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dk. Mehmet Gulluoglu, amesema lengo la kuisaidia Taasisi ya Karume vifaa vya 3D ni Kuitaka Taasisi hiyo kutoa  wataalamu wanaoendana na wakati wa sasa ambao watakuwa na ujuzi wa aina nyingi. 

Aidha, Balozi Mehmet amewataka  wanafunzi kuitumia vyema studio ya 3D, pamoja na kuutumia vizuri  wakati,  na mitandao kwa lengo la kujifunza na sio kupoteza muda. 

Hata hivyo amewapongeza viongozi wakuu wa Zanzibar na Tanzania pamoja na uongozi wa Taasisi kwa jitihada za maendeleo zinazoendelea kufanyika na kuahindi kuendeleza ushirikiano baina ya Uturuki na Tanzania ili kufanikisha mipango ya maendeleo ikiwemo Sekta ya Elimu.









No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.