Habari za Punde

Tanzania Yaendelea Kujidhatiti katika Uzuiaji wa Utakasishaji wa Fedha Haramu

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb),akifuatilia baadhi ya matukio katika ufunguzi wa Mkutano wa 23 wa Baraza la Mawaziri na Maafisa Waandamizi wa Umoja wa  nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa kudhibiti Utakasishaji  Fedha Haramu unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hotel ya Cresta Mowana, nchini Botswana. Pembeni kwa Mhe. Chande ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) katikati akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa kwanza kushoto) wakipata maelezo kutoka kwa Afisa itifaki Mkuu wa ESAAMLG Bw. Boiki Ramatho nje ya Ukumbi wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri na Maafisa Waandamizi wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika unaofanyika Mjini Kasane -Botswana.

Na Ramadhani Kissimba, Botswana

Tanzania imekuwa mojawapo ya nchi zilizo Mashariki na Kusini mwa Afrika zilizopiga hatua kubwa katika udhibiti wa utakasishaji fedha haramu na uzuiaji wa silaha za maangamizi na ufadhili wa ugaidi nchini.

 

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amesema hayo katika Mkutano wa 23 wa Baraza la Mawaziri na Maafisa Waandamizi wa Umoja wa  nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu (Eastern and Southern Africa Anti Money Laundering Group (ESAAMLG), unaofanyika katika mji wa Kasane, nchini Botswana.

 

Mhe. Chande alisema Tanzania ipo katika hatua nzuri hasa katika suala zima la kupambana na ugaidi, utakasishaji fedha haramu na uzuiaji wa silaha za maangamizi.

 

‘’Niwatoe shaka ndugu zangu Watanzania kuwa nchi yetu ipo katika hatua nzuri katika suala zima la kupambana na utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa kigaidi pamoja na ufadhili wa silaha za maangamizi’’ alisema Mhe.Chande.

 

Aidha, Mhe. Chande alisema kuwa Mkutano huo ulitumika kupitia mpango kazi wa Jumuiya ya ESAAMLG na kuangalia ni namna gani wanachama wanaweza kupunguza matumizi ya kuendesha Jumuiya hiyo hasa kwa kuanzisha utaratibu wa kuendesha shughuli za Jumuiya kwa kutumia njia za kieletroniki (Paperless).

 

Mhe. Chande aliongeza kuwa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wamekubaliana kuongeza ajira ya vijana ambao watasaidia katika sekretarieti ya Jumuiya ili kazi za ESAAMLG ziweze kutekelezwa kwa ufanisi zaidi, na kuwataka Watanzani kuchangamkia fursa hizo za ajira kwa sababu Tanzania ni nchi mojawapo itakayofaidika na ajira hizo na kuongeza kuwa uwepo wa Watanzaia katika Jumuiya utasaidia kujifunza mambo mengi na kupata fursa ya kufaidika kama nchi.

 

‘’Na imani  kubwa kuwa Watanzania wataingia na kuwa sehemu ya ajira hizo na kutakuwa na mafanikio makubwa sana, na uwepo wao ndani ya Jumuiya tutajifunza mengi ambayo yatanufaisha Taifa letu’’ aliongeza Mhe.Chande.

 

Mkutano wa 23 wa Baraza la Mawaziri na Maafisa Waandamizi wa Umoja wa  nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu (Eastern and Southern Africa Anti Money Laundering Group (ESAAMLG) umehudhuriwa na nchi wanachama 17 zilizo Mashariki na Kusini mwa Afrika, Mkutano ujao utafanyika nchini Kenya.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.