Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj.Othman Masoud Amejumuika na Wananchi wa Kichangani Tumbatu

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, amesema Hafla za Kidini, zikiwemo za Maulid ni Nyenzo Muhimu za kuirejesha Jamii katika Mshikamano na Kujenga Umoja wa Nchi.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Usiku wa kuamkia Leo Jumapili, huko Viwanja vya Masjid Noor, Msikiti uliopo Kichangani, Wilaya Ndogo  Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati akitoa Nasaha zake kwa Waumini wa Kiislamu, katika Hafla ya Maulid Matukufu ya Mwaka, ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Amesema Hafla za aina hiyo zinazolenga pia kutunza Mila na Silka za asili, za Watu wa Visiwa vya Unguja na Pemba, Tanzania  na Mwambao wote wa Afrika Mashariki, ni muhimu sana, kwa kuzingatia kwamba ni Shirikishi na zinazowaweka pamoja Watu wote, bila kujali itikadi na tofauti zao.

"Tupo hapa tumekusanyika baina yetu, huwezi kumjua ACT-Wazalendo; huwezi kumjua CCM; huwezi kumjua nani Mtawala, wala Mtu kwa Cheo chake; bali tunachojali ni Umoja na kuenzi utamaduni wetu na pia kuheshimu Miongozo ya Kiongozi wa Umma huu, Mtume Muhammad (S.A.W.), amesema Mheshimiwa Othman.

Hivyo amesema jambo lililo bora zaidi ni kwa jamii yote kuzingatia na kuendeleza umoja na mshikamano, bila kujali itikadi zinazowagawa, zikiwemo za Vyama vya Siasa, na hivyo kushikamana kukupitia mambo ambayo ni alama na utambulusho wa utamaduni wa asili sambamba na kuheshimu mila, silka na maadili mema.

Amefahamisha kuwa kuporomoka kwa maadili sasa, kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na jamii kudharau uasili, hali ambayo inawatupa vijana katika mkondo wa mageuzi ya maisha duniani, ambao wimbi lake siyo salama.

Mheshimiwa Othman amekuwepo Tumbatu kwa Ziara Maalum ya Siku Mbili, iliyoambatana pia na Ushiriki wa Hafla za Maulid, Kuwatembelea na Kuwajulia Hali Wagonjwa, na pia Kujumuika pamoja na Wazee wa huko akijiunga nao katika Barza za asili na  kupata 'kubaariz'  kwa kubadilishana mawazo na hata 'kahawa' pamoja nao.

Kabla ya kujiunga katika 'Dhikri Mashuhuri ya Kigumi na Kupokea Zafa' kutoka kwa Watu wa Kijiji hicho, Mheshimiwa Othman ametembelea Maeneo mbalimbali na kujionea mambo mengi ya kuenziwa, na uasili katika Shehia ya Gomani Tumbatu.

Akibadilishana Mawazo na Wazee, Mheshimiwa Othman amesisitiza  umuhimu wa kuwarithisha vijana mambo ya msingi ambayo jamii hapo zamani iliyaenzi kwa nia ya kulinda maadili mema, akisema, "mtu asiyekuwa na utambulisho inakuwa wepesi kwake kupoteza kila kilicho chake na kuachana na utamaduni wake, na ikibidi kupoteza hata Misingi ya Dini yake".

Aidha ameeleza kwamba ili jamii na Nchi kwa ujumla, zisiingie katika lawama na majuto makubwa ya baadae, ni wajibu kukilea kizazi, na kuwatunza vijana wa kike na wa kiume, kwa kuwachunga na kuwashirikisha kikamilifu katika mambo ya kimaadili, ambayo yanalenga kuenzi utamaduni wa asili.

Mheshimiwa Othman amekhitimisha Khutba yake kwa kuwakumbusha akinamama wajibu walionao wa msingi, katika kufanikisha malezi mema ya watoto, ya kwamba wao ni sehemu muhimu kutokana na maumbile, huruma na ukaribu wao ndani ya familia.

Naye, Khalifa wa Twarika ya Qaadiriya Zanzibar, Sayyid Omar Qullatain, katika Salamu zake amesema ni kheri kubwa kuona Vongozi wa Nchi wanatoa mwamko katika kuuungamkono Hafla Muhimu za Malezi na za Kimila, zikiwemo za Mazazi Matukufu ya Mtume Muhamad (S.A.W).

"Hili ni jambo la kuendelezwa na kuheshimiwa kwa maslahi ya Jamii ya Tumbatu na Taifa kwa Ujumla", amesema Sayyid Qullatain.

Hafla hiyo iliyowahusisha Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Jamii na Vyama vya Siasa, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, imewajumuisha Watu kutoka Maeneo ya Visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Tanzania Bara, na baadhi  yao kutoka Nchi za Jirani.

Wengine ni pamoja na Masheikh, Waumini, 'Twarika' mbalimbali, Vijana wa Madrasa, Walimu na Wanafunzi, Makundi ya Wananchi, Kike kwa Kiume, Wakubwa na Wadogo, ambao awali walishiriki kumpokea na kumkaribisha Mheshimiwa Othman, na hatimaye pia kujumuika katika Maadhimisho hayo.

Kwa ujumla Tumbatu imekuwa Sehemu muhimu ya Zanzibar, Tanzania na Bara la Afrika katika Mwendelezo wa Maadhimisho hayo,, mwenendo ambao umechukuliwa na kurithishwa kwa kizazi kipya, kama sehemu muhimu ya Utamaduni wao wa asili.

Kitengo cha Habari,

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,

Oktoba 15, 2023.








No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.