Habari za Punde

Wizara ya Kilimo,Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo Zanzibar Yaahidi Kuunga Mkono Juhudi za Wadau wa Kilimo

Katibu wa kikundi cha Tumaini la kijani Ali Shauri akizungumza na wafadhili wa mradi wa agriconnect kuhusiana na bustani za nyumban (kitchen garden) wakati walipowatembelea kuangalia maendeleo ya mradi huo,huko Chuini Wilaya ya Magharibi “A”.

Na Fauzia Mussa ,     Maelezo

Wizara ya Kilimo ,Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar imesema uwepo wa miradi ya kilimo  kunapelekea kuikomboa jamii kiuchumi.

 

Akizungumza wakati wa ziara ya wadau wa mradi wa Agri connect  kuangalia utekelezaji wa mradi huo  Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo Pemba Mhandisi Idris Hassan Abdulla amesema kupitia mradi huo jamii imeweza kunufaika kwa  kujiongezea kipato pamoja  na kupata lishe nzuri kwaajili ya familia.

 

Alifahamisha  kuwa  Mradi huo  una  lengo la kuwainua wakulima wa mbogamboga , viungo,pamoja na wajasiriamali wanaojishuhulisha na utengenezaji wa majani ya  chai na kahawa,hivyo Wizara itaenedelea kuunga mkono juhudi za wadhamini wa mradi huo ili kufikia malengo yalioyotarajiwa. 

 

Mapema  ameishukuru  Jumuiya ya umoja wa ulaya kwa kuwekeza fedha zao katika mradi huo unaolenga kutoa ajira hasa  kwa wanawake na vijana.

 

Kwa upande wake Meneja Mkuu mradi wa viungo Simon Makobe alisema lengo la ziara hiyo ni kuangalia changamoto zinazowakabili watekelezaji wa miradi ya agri connect na kuweza kuzipatia  ufumbuzi.

 

 Aidha aliishukuru Wizara ya Kilimo kwa kusimamia shughuli zote zinazofanyika chini ya mradi huo pamoja na  Jumuiya ya Ulaya ambayo imeamini kutoa fedha na kuziwekeza kwa wajasiariamali wakiwemo  wakulima wa mbogamboga, matunda na viuongo.

 

Sambamba na hayo aliwataka wakulima kushirikiana kwa pamoja katika kilimo kwa  kuzalisha bidhaa zinazofanana ili kurahisisha kupata masoko.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Katibu wa kikundi cha Tumaini la Kijani Ali Shauri  na mkulima wa Viungo Aviwa walisema kwasasa wamekuwa wakipunguza gharama za matumizi kwaajili ya mlo kwani kilimo kinawasaidia kupata mahitaji ya chakula na  mbogamboga.

 

"Sasahivi kina mama  hawanunui tena mboga,tungule ,bamia,wala nyanya zote tunapata kupitia bustani zetu za nyumbani"Katibu huyo

 

Walisema kupitia mradi huo jamii  imepata  elimu juu  ya mbinu bora za kilimo hai hivyo kwasasa wanajipatia chakula salama kwani wanarutubisha vilimo vyao kwa kutumia mbolea asili ikiwemo kinyesi cha Ng’ombe.

 

Aidha walisema awali jamii  ilikua ikipanda bustani za maua kama pambo lakini baada ya kupata elimu  wameanza kupunguza upandaji wa maua na wengine kuoondoa kabisa nakuweka bustani za mbogamboga (kitchen garden ) pembezoni mwa nyumba zao ili kupunguza gharama za mlo.

 

Hivyo waliwashauri Vijana na Wanawake kuacha kukaa bila ya kujishughulisha  na badala yake kujiunga na vikundi vya ujasiriamali na  kuanzisha kilimo kitakachowapatia kipato na   kupunguza gharama za maisha .

 

Mbali na mafanikio hayo wakulima hao wanakabiliwa na uhaba wa maji,pamoja na masoko ya nje.

 

Ziara hiyo iliyoambatana na ujio wa ujumbe wa jumuiya ya umoja wa Ulaya ,watekelezejai wa miradi ya Agri connect Zanzibar na Tanzania Bara, timu ya ushauri wa mradi Tanzania wakishirikiana na Wizara ya kilimo na fedha Zanzibar ilifanikiwa kutembelea kikundi cha Tumaini la kijani Chuini,Shamba la  Viungo na matunda Kizimbani na kiwanda cha kutengeneza majani ya Chai Amani Zanzibar.





Mkulima wa viungo(spices) na matunda Aviwa akielezea  maendeleo ya  kilimo hicho wakati alipotembelewa na wadau wa mradi wa Agri connect huko Kizimbani Wilaya ya Magharibi “A”.

Wadau wa Mradi wa Agri connect wakiangalia ufungaji wa majani ya chai wakati walipotembelea kiwanda hicho huko Amani Wilaya ya Magharibi “A”.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.