Habari za Punde

ZFDA Yatoa Elimu ya Maji Safi na Salama Siku ya Chakula Duniani

Afisa habari Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi ZFDA Zuwena Makame  akitoa elimu kwa wanafunzi wa Skuli ya kinyasini juu ya umuhimu wa kutumia maji safi na salama  wikiaadhimisha siku ya usalama wa chakula ambayo hufanyika kila ifikapo Oktoba 16 ya Kila mwaka duniani kote,hafla iliyofanyika Skuli ya Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mkaguzi wa chakula ZFDA Mwajuma Kombo Ali akiwasilisha mada ya maji safi na salama kwa wanafunzi wa Skuli ya Kinyasini katika siku ya chakula ambayo hufanyika  kila ifikapo Oktoba 16 ya Kila mwaka duniani kote.
Wanafunzi wa Skuli ya  kinyasini wakifuatilia mafunzo ya maji safi na salama katika siku ya usalama wa chakula ambayo hufanyika kila ifikapo Oktoba 16 ya Kila mwaka duniani kote.

Mwanafunzi wa kidatu cha pili Skuli ya Kinyasini Asma Haji akiuliza suala kwa maofisa wa ZFDA (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wanafuzi hao juu ya maji safi na salama katika maadhimisho ya siku ya Chakula ambayo hufanyika kila ifikapo Oktoba 16 ya Kila mwaka duniani kote,hafla iliyofanyika Skuli ya Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja.

PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzia Mussa,      Maelezo

 

Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar ZFDA imeitaka Jamii kutumia maji safi na salama wakati wa  kuandaa,kutumia na kusindika chakula ili kujikinga na maradhi mbalimbali ikiwemo kipindupindu.

 

Akizungumza na Wanafunzi wa Skuli ya Kinyasini  Mkaguzi wa chakula ZFDA Mwajuma Kombo Ali wakati akitoa elimu  ya maji safi na salama katika maadhimsho ya siku ya chakula amesema endapo jamii itatumia maji yasio salama wakati wa uandaaji wa chakula itapelekea uchafuzi na kusababisha madhara kwa mtumiaji.

 

Amesema ili maji yabaki kuwa  safi  na salama ni lazima yawe yameepukana na uchafuzi wa aina zote  ikiwemo wa kibakteria , kemikali za sumu, pamoja na uchafuzi wa kifizikia kama vile mawe ,mchanga au dongo.

 

Alifahamisha kuwa sio rahisi kutambua usalama wa maji kwa macho ya kawaida hivyo aliitaka jamii kuwa na utaratibu wa kutibu maji kwa kuyachemsha au kuweka dawa maalum (waterguard) ili kulinda afya zao.

 “kwa macho ya kawaida utajua kama maji haya ni safi kwa sababu hutaona kitu chochote lakini  ili kujua kama maji hayo ni  salama lazima yapelekwe maabara kwaajili ya uchunguzi.”alifahamisha Ofisa huyo

 

Alisema kuwa visima na mifereji ni miongoni mwa vyanzo vya maji safi na salama hivyo aliitaka jamii kuyahifadhi maji hayo katika vyombo safi na kuyaweka mbali na mionzi ya jua kwani mionzi hiyo huondoa ubora na kutengeneza sumu inayosababisha madhara kwa mtumiaji.

Vilevile aliitaka jamii kuacha tabia ya kutumia maji ya mito na maziwa kwani sio salama kwa matumizi ya binaadamu.

“sio maji tu bidhaa yoyote ya chakula haitakiwa kuwekwa juani,mionzi ya jua hutengeneza sunu katika vyakula, baada ya kunua soda unanunuwa sumu kwa pesa yako mwenyewe utakuwa unanunua maradhi”alifahamisha Mkaguzia huyo.

Mapema akitoa maelezo kuhusu Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi ofisa habari ZFDA Zuwena Makame amesema Taasisi hiyo ipo chini ya Wizara ya Afya na inafanaya kazi kwa mujibu wa sheria Na.2/2006 na marekebisho yake Na.3/2017 ikiwa na  jukumu la kulinda na kuimarisha Afya za wananchi.

Amesema katika kuunga mkono maadhimisho ya siku ya chakula Duniani ZFDA imeamua kutoa elimu hiyo ikiamini kuwa  maji ni chakula.

 

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo mwanafunzi Khalid Othman na Asma Haji wamesema kupitia mafunzo hayo wameweza kujua njia za  kutunza ,kuhifadhi na kutibu maji ili kuepukana na madhara yanayotakana na maji yasiosafi na salama.

Hata hivyo wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo na kusema watakua mabalozi wazuri wafikapo majumbani ili kuhakisha jamii iliyowazunguka haipati maradhi yatokanayo na matumizi ya maji yasio salama.

 

Maadhimsho ya siku ya  Chakula Duniani hufanyika  Kila ifikapo  Oktoba 16 ambapo kauli mbiu kwa mwaka huu ni “Maji Ni uhai,Maji ni chakula asiachwe mtu nyuma

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.