Habari za Punde

Mhe.Simai Azindua Mradi wa Umeme Kijiji cha Upenja Chokwe

Na Ali Issa.   Maelezo.  29/12/2023.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe.Simai Muhamed Said amesema Mradi wa Umeme Vijijini ni kichocheo cha ukuaji Uchumi Nchini. 

 

Ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Umeme katika Kijiji cha Upenja Chokwe Wilaya ya Kaskazini, ikiwa ni shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Amesema Wananchi wa Kijiji hicho kwa muda mrefu walikosa huduma ya Nishati ya Umeme na kupelekea kushindwa kuendeleza harakati za Maendeleo ikiwemo Kilimo.

 

Amefahamisha kuwa katika kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji walilazimika kutumia Janareta jambo ambalo lilikuwa linawasabishia hasara kubwa hivyo kupatikana kwa Umeme huo kutawawezesha Kulima Kilimo cha Mbogamboga na kupeleka katika Masoko ya Utalii.

 

Amewataka Wananchi kutumia Umeme huo kwa uangalifu ili waweze kuhifadhi Mazao, Samaki, Biashara za Kilimo na Mazao ya  Baharini sambamba na kulinda Miundombinu ya Umeme ili isifanyiwe uharibifu.

 

Nae Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Khamis Ahmada Fakih alisema utekelezaji wa Mradi huo ni kuhakikisha huduma ya Umeme inafika katika maeneo ambayo hadi leo haujafika na kufanya maboresho maeneo yanayopata Umeme mdogo.

 

Alisema zaidi ya shillingi milioni miambili na hamsini  zitatmika katika kukamilisha Mradi huo kwa kuweka njia za usambazaji  Umeme mkubwa kilovolt 33kv ambapo una urefu wa kilo mita 3, kuweka Transfoma yenye ukubwa wa Kilovolt 200 kv.

 

Aidha alisema kuna maombi mengi katika maeneo ya Kilimo hivyo dhamira yao ni kuwafikishia huduma hiyo wananchi wote.

 

Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Rashid Hadid Rashid alisema Mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025katika kuhakikisha Wananchi wote wanapata huduma ya Umeme katika maeneo yao.

Alisema Serikali imefanya Maamuzi makubwa kwa Wanakiji Cha Upenja Chokwe kuwapatia huduma hiyo na juhudi zitaendelea kwa Vijiji vyengine 42 vilivyobaki katika Mkoa huo ili Wananchi wote wapate Nishati hiyo muhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.