RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Serikali ya Saudi Arabia kwa
jitihada kubwa wanayoitoa Tanzania kuungamkono miradi mbalimbali ya maendeleo
ikiwemo sekta ya Afya, maji, miundombinu ya barabara na kusaidia uzalishaji
umeme.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo
Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania,
Mhe. Yahya Ahmed Okeish aliefika
kujitambulisha.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwepo
kwa ubalozi huo nchini ni mwendelezo wa ushirikiano mwema uliopo baina ya
Tanzania ikiwemo Zanzibar na Saudi Arabia.
Dk. Mwinyi aliipongeza
Serikali ya Saudi Arabia kwa ushirikiano wanaoutoa Tanzania Bara kwenye uzalishaji
wa umeme, kuungamkono ujenzi wa barabara ya Wete, Pemba pamoja na kusaidia ukarabati
mkubwa kwenye hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ambayo inatarajiwa kufanya upasuaji
mkubwa zaidi mara baada ya kumalizika kwa ukarabati wa vyumba vya upasuaji
vinavyotarajiwa kuwa na vifaa vya kisasa kwa msaada wa Mfuko wa Saudia.
Pia, Rais Dk. Mwinyi, aliikaribisha
Serikali ya Saudi Arabia kuwekeza kwenye Shamba la Makurunge, Bagamoyo,
linalomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambalo linafaa kwa
uwekezaji wa Kilimo, Uvuvi na Utalii.
Halikadhalika, Dk. Mwinyi
aliendelea kuishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa msaada mkubwa kwa Zanzibar
kupitia sekta ya afya ambapo imetoa timu ya madaktari wa upasuaji iliyojitolea
kuweka kambi na kuwatibu Wazanzibari.
Aidha, Dk. Mwinyi
aliipongeza timu ya madaktari 21 kutoka Saudi Arabia waliojitolea kuweka kambi
ya matibabu kwenye jimbo la Gando kisiwani Pemba ambako waligundua zaidi ya
kesi 680 na kufanya upasuaji.
Alisema, kambi za matibabu ni
moja ya eneo muhimu la ushirikiano uliopo baina ya Zanzibar na Saudi Arabia
kwani zimekua na msaada mkubwa kupunguza changomo nyingi kwenye sekta ya afya
nchini.
Mbali na sekta ya afya pia
Rais Dk. Mwinyi aligusia maeneo mengine ya ushirikiano wao ikiwemo uwekezaji,
biashara, uvuvi na kilimo cha Samaki kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu.
“Tunahitaji uwekezaji
zaidi, hasa kwenye Sekta ya Uchumi wa Buluu, nchi yetu imezungukwa na bahari, Sera
yetu kuu ya uchumi ni ‘Uchumi wa Buluu’,
hivyo tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye eneo hilo, kupitia uvuvi na
kilimo cha Samaki” Dk. Mwinyi alimweleza Balozi huyo.
Rais Dk. Mwinyi aliipongeza
tena Saudi Arabia kuwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa maonesho makubwa ya biashara
duniani, (Expo 2023).
Naye, Balozi, Yahya Ahmed
Okeish alisema Saudi Arabia imekua na msaada mkubwa kwa bara la Afrika ikiwemo Tanzania
ambapo Zanzibar pia itanufaika kwa kiasi kikubwa na fursa nyingi baada ya kusainiwa
kwa makubaliano ya mamilioni ya dola za Marekani zilizoelekezwa Afrika.
Alisema, Tanzania na Saudi
Arabia kwa muda mrefu, zimekua zikibadilishana uzoefu baina yao kupitia sekta
mbalimbali za ushirikiano wao.
Balozi Yahya pia
aliambatana na timu ya mataktari wa upasuaji 21 kutoka Saudi Arabia ambao
walikuwepo kisiwani Pemba kwenye jimbo la Gando walikoweka kambi ya matibabu
kwa maradhi mbalimbali.
Akizungumza kiongozi wa timu
ya madaktari hao, Dk. Aiman Al Soluman alisema, waligundua kesi 689 kati ya
wagonjwa wengi waliojitokeza kwenye kambi ya matibabu yao, kati yao kesi 303
zilifanyiwa upasuaji.
Alisema, wagonjwa wa upasuaji
wa jumla walikua 124 kati yao 76 walifanyiwa upasuaji wa jumla, pia alieleza waligundua
matatizo ya mfumo wa mkojo kwa watoto na watu wazima kwa kesi 112 na kesi 78
zilifanyiwa upasuaji.
Dk. Al Soluman pia aligusia
operesheni ya viungo vya mwili zilivyopotea au kupata athari ikiwemo makovu makubwa,
(plastic surgery) alisema walipata kesi 60 na 56 zilifanyiwa upasuaji.
No comments:
Post a Comment