SERIKALI ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imewaonya waanchi kutojenga maeneo karibu na miundombinu ya barabara,
maji na umeme ili kupunguza gharama kwa Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa onyo
hilo alipojumuika pamoja na waumini wa Kiislamu kwenye Ibada ya Sala ya Ijumaa,
iliyoambanata na ufunguzi wa Msikiti wa ijumaa, Masjid Sheikha Naima bint Sultan Al
Qasmi pamoja na madrsa, Tomondo Wilaya
ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema nia ya Serikali ni kufikisha miundombinu ya barabara maeneo yote
yanayohitajiwa na jamii lakini wakati mwengine Serikali inashindwa kutokana na
gharama kubwa za ulipaji wa fidia wananchi waliojenga kiholela karibu na maeneo
ya barabara.
Alisema, mara nyingi Serikali hukumbana na gharama kubwa za ulipaji wa
fidia kwa wananchi kuliko gharama za kutengeneza miundombinu hiyo, alishauri
kutolewe vibali maalum kwa wananchi watakaojenga karibu na barabara.
“Mara nyingi matatizo hayo yanatukuta kwasababu watu wajenga ovyo,
hawachi hata njia ya kupita gari, anakuja mtu anaweka jengo lake katikati ya
barabara, inakua mtihani unapotaka kupitisha miundombinu inakubidi uanze kulipa
fidia kwanza, pesa nyingi zinaingia kwenye fidia kabla hujaanza ujenzi wa hiyo
barabara”
“Wananchi muwe waangalizi wenyewe, anaejenga sehemu itakayopita barabara
mumzuie, hii itawaathiri nyinyi wenyewe msipoifanyia kazi, ombi langu kwenu,
watu waambiwe wajenge kwa vibali maalumu, wasijende ovyo wala sehemu zitakazo
pita barabara” aliisihi jamii.
Hivyo, Al hajj Dk. Mwinyi ameitaka jamii kuwa mfano bora kwa kukatazana
wenyewe kwa wenyewe kutojenga maeneo karibu na miundombinu ya barabara ili kuipunguzia
mzigo mzito Serikali.
Al hajj Dk. Mwinyi pia aliitaka jamii kuwafundisha mema ya dini watoto ili
waijue dini yao, pamoja na kuipongeza taasisi ya “Al Noor Charitable Agency for
the need” kwa kushughuhulika na masuala mengi ya jamii wakiwemo watoto yatima,
wajane, watu wazima na wenye ulemavu pamoja na kujishughulisha na huduma za
jamii, ikiwemo elimu, maji (visima), kujenga misikiti mikubwa yenye hadhi ya
juu na madrasa.
Pia, Al hajj Dk.
Mwinyi ameitaka Misikiti mengine kuiga mifano mema kwa kushughulikia na
kuyafanyia kazi matatizo yanayoikabili jamii kwenye mitaa yao pamoja na kufanya
ibada kwa wingi.
Sambamba na kuwataka
waumini wanaoitumia misikiti hiyo, kuitunza na kuikarabati kwa huduma zote
zitakazohitajika zikiwemo maji, umeme, kuwalipa wanaohudu misikiti na
matengenezo mengine ya lazima.
“Misikiti ifundushe
vijana na watoto dini yao, ukiachia mbali kufanya ibada pekee, pia kuitumia
vizuri misikiti hiyo” alitoa msisitizo.
Hata hivyo, Al hajj
Dk. Mwinyi alieleza jinsi alivyolipokea ombi la ujenzi wa barabara iliyopita
kwenye masjidi hiyo na kuahidi kuitengeneza ipitike kwa wepesi.
Akitoa shukurani kwa
niaba ya taasisi ya kiislam ya Al Noor ya Zanzibar “Al Noor Charitable Agency
for the need” Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sheikh Luay Mohamed Makhfoudh alisema,
ufunguzi wa msikiti huo ni maadhimisho ya miaka 20 ya huduma kwa jamii ya
Zanzibar waislamu na wasiokua waislamu zinazotolewa na taasisi hiyo tokea
ilipozinduliwa kwake mwaka 2003.
Alisema, Masjid Naima
bint Hamed Al Qasmi ni msikiti wa 28 kati ya misikiti iliyojengwa na taasisi
hiyo, unauwezo wakuchukua hadi waumini 880 ambapo kwa mwaka huu pia wamejenga
misikiti mitatu ukiwemo huo na mengine midogo iliyojengwa maeneo ya Kama na
Koani.
Alisema, misikiti 20
kati ya 28 inaitwa Markadhi Islami mbali na kutoa huduma za ibada pia ina
madrsa zenye uwezo wakuchukua hadi wanafunzi 300, zinazosomesha tahfidh Quran
na masomo ya kiingereza na hisabati ili kuongeza nguvu kwenye masomo hayo
nchini.
Alisema, wakati wa
jioni misikiti hiyo hutoa darsa kwa wanawake na usiku madrsa za misikiti hiyo
hutumika kwa mabweni ya wanafunzi kupata misaada ya kujifunza masomo yao ya
skuli ili kutoa matokea mazuri masomo yao ya skuli.
Pia alieleza madrsa
zao zina wanafunzi zaidi ya 7,000 kati ya hao 550 ni yatima, hivyo, aiitaka
jamii kusajili yatima kwenye taasisi za “Al Noor Charitable Agency for the
need” hasa waliofiliwa na baba zao ambao husaidiwa kwa huduma majumbani mwao,
kusomeshwa hadi nje ya nchi kwa mataifa ya India, Madina, Morocco, Sudan,
Uturuki na Yemen.
Taasisi ya “Al Noor
Charitable Agency for the need” pia wanashughulikia watu wenye ulemavu, wajane,
na watu wazima waliosajiliwa na taasisi hiyo hupewa kipaombele inapopatikana
riski ya sadaka.
Mapema akisoma risala
ya ufunguzi wa Masjid Sheikha Naima bint Sultan Al Qasmi, pamoja na madrsa
yake, Ustadhi Abdul Mabrouk Kitwana kwa niaba ya wananchi wa Tomondo, walimshukuru
Al hajj Dk. Mwinyi kwa mapenzi yake ya kujumuika pamoja nao kwenye ibada ya
sala ya Ijumaa sambamba na kufikisha shukurani zao za dhati kwa mfadhili wa
msikiti huo, Sheikha Naima bint Sultan pamoja na taasisi ya “Al Noor Charitable
Agency for the need” kwa kuishirikisha kikamilifu jamii ya Tomondo kwenye
ujenzi wa msikiti huo.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment