Habari za Punde

Shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Aweka Jiwe la Msingi Hoteli ya Nyota Tano

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla akiweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Hoteli ya Mada Iliyoko Michanvi Kae Zanzibar  ikiwa ni katika Shamra Shamra za kutimia Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu  ya Zanzibar.  Imetolewa na Kitengo cha  Habari cha (OMPR)


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Awamu ya Nane (8) kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050, Sera na Mikakati mbali mbali imekuwa ikiendelea kuimarisha Sekta ya Uwekezaji nchini kwa kuweka mazingira bora ambayo yanawavutia wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar.

Ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Hoteli ya Mada yenye hadhi ya Nyota Tano (5) iliyoko Michanvi Kae Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni katika shamra shamra za kutimia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha na kujenga miundombinu ya Barabara na Viwanja vya ndege sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma za nishati, maji safi na salama na huduma nyengine za kijamii ili kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji.

Mhe Hemed amefahamisha kuwa Mradi wa Ujenzi wa Hotel Mada unaomilikiwa na kampuni ya MADA HOTEL TANZANIA LIMITED hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu USD 6,500 utakaokuwa na vyumba mia moja(100) vya kulaza wageni na kusaidia kuzalisha ajira zaidi ya mia mbili (200) kwa vijana ambapo amewataka wawekezaji wa mradi huo kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakaazi wa Michanvi na vijiji jirani.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais amewasihi vijana ambao watapata ajira katika mradi huo kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii ili waendelee kuaminika katika majukumu watakayopangiwa sambamba na kuwataka wawekezaji wa mahoteli kutekeleza wajibu wao hasa katika kulipa kodi stahiki, kuwatendea haki wafanyakazi wao pamoja na kushirikiana na wananchi wanaoishi  maeneo yanayowazunguka ili kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, kazi, Uchumi na Uwekezaji Mhe Mudrik Ramadhan Soraga amewataka wale wote waliopewa maeneo kwa ajili ya shuhuli za Uwekezaji kuyatumia maeneo hayo kama walivyopangiwa na Serikali na kuacha tabia ya kutoyatumia maeneo hayo na hatimae kuwa magofu jambo ambalo linarejesha nyuma malengo ya serikali.

Soraga amesema Sheria mpya ya uwekezaji ambayo inatarajiwa kusainiwa hivi karibuni imeainisha hatua  zitakazochukuliwa kwa muwekezaji ambaye atazuwia eneo la uwekezaji pasipo kulifanyia shuhuli stahiki ikiwa ni pamoja na kurudishwa serikalini eneo hilo na kupewa wawekezaji wengine kwa maslahi ya taifa.

Amesema kuwa Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar(ZIPA) inafanya kazi kwa haraka na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma katika mamlaka hiyo unakuwa wa rahisi na kwa wakati muafaka.

Mapema Mkurugenzi Mtendajeji wa Mamlaka ya uwekezaji Zanzibar Ndugu sharif Ali Sharif amemshukuru muwekezaji kwa kuendelea kuiamini Zanzibar na kuja kufanya uwekezaji mkubwa ambao utatoa ajira nyingi kwa wazawa na kuipatia pato Serikali ya Zanzibari jambo litakalosadia katika kukuza uchumi wa Taifa letu.

Amesema mradi huo wa hoteli yenye hadhi ya nyota tano utagharimu jumla ya Dola milioni 30 na kutoa ajira zaidi ya watu 250 jaambo ambalo utakuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Nae Muwekezaji wa Shukurani Palece Hotel Bwana TARLOCHAN MHANJAN amesema sababu kubwa ya kuja kuwekeza Zanzibar ni uzuri wa Visiwa vyenyewe na hali ya hewa inayopatikana, mazingira mazuri na ushirikiano wanaopatiwa na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na utayari wa wananchi wake kushirikiana na wawekazaji mambo ambayo yanawapelekea kufanya kazi zao kwa utulivu mkubwa.

Amesema kuwa Shukurani Palece Hotel inathamini na kuunga mkono Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ndio msingi wa uwepo wa Amani na Utulivu uliosababisha uwepo wao hapa Visiwani Zanzibar.

Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.