Habari za Punde

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA REDIO MPIMBWE JIMBONI KAVUU

 

Waziri Mkuu Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza wakati akizindua Redio ya Mpimbwe Fm katika halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoa wa Katavi tarehe 25 Februari 2024. Kushoto ni Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda.
Waziri Mkuu Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa akiangalia namna Redio ya Mpimbwe Fm inavyofanya kazi alipoizindua rasmi katika halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoa wa Katavi 
                                                             

Na Munir Shemweta, MLELE.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasim Majaliwa Majaliwa amezindua Redio ya Mpimbwe fm inayomilikiwa na Halmashauri ya Mpimbwe iliyopo jimbo la Kavuu wilayani Mlele mkoa wa Katavi na kutaka redio hiyo kutumika kutangaza shughuli za maendeleo.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 25 Februari 2024 katika halmashauri hiyo mbele ya Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kavuu ambapo Mhe, Majaliwa alikuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano huo ambapo mbunge wake Mhe, Geophrey Pinda aliwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Kipindi cha kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2024.

Mhe, Majaliwa ameitaka redio hiyo ya Mpimbwe kutoa nafasi kwa wakuu wa idara za halmashauri ya Mpimbwe kuelezea kazi zinazofanywa na halmashauri hiyo sambamba na idara nyingine za serikali ili wananchi wafahamu.

                                                                                              

"Unaweza kumuita mkuu wa idara ya elimu katika kipindi ili aeleze umuhimu wa masuala mbalimbali yanayofanywa katika sekta ya elimu kwenye jimbo hilo la Kavuu pamoja na halmashauri ya Mpimbwe kwa ujumla" alisema

 

‘’Wananchi wanaweza kuitumia vizuri redio namna wanavyofurahishwa na kazi zinazofanyika na wakati huo wakuu wa idara wakaitumia kueleza mikakati iliyopo katika halmashauri hiyo  kama vile masuala ya afya na elimu’’n alisema Mhe, Majaliwa.

 

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko alimueleza Waziri Mkuu kuwa, kuzinduliwa kwa Redio hiyo kunatoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri na maeneo jirani kupata taarifa za uhakika na  sambamba na urahisi wa kufikisha ujumbe kwa jamii.

 

‘’ Redio uliyoizindua ni ya kwanza kumilikiwa na taasisi ya serikali katika mkoa huu na ujio wa redio hii ni mkombozi kwa mkoa huo kwa kuwa itasaidia kufikisha ujumbe wa serikali kwa wananchi sambamba na kupokea kero na changamoto za wananchi’’. Alisema Mwanamvua Mrindoko.

 

Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda ameeleza kuwa uzinduzi wa redio Mpimbwe ni mkombozi kwa halmashauri ya Mpimbwe na wananchi wa jimbo lake kwa kuwa watapata fursa ya kutumia katika shughuli za maendeleo.


Aidha, alisema pamoja na mafanikio makubwa ya upatikanaji redio bado kuna  changamoto kadhaa kama vile halmashauri yake kuwa na upungufu mkubwa wa watumishi ambapo kwa sasa ina watumishi 892 tu sawa na 43% ya mahitaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.