Habari za Punde

ASEMA CCM ITATOA KIPAUMBELE KWA VIONGOZI WANAOTATUA CHANGAMOTO

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akiwahutubia Wanachama wa CCM Jimbo la Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba katika hafla ya ugawaji wa Pikipiki na mitungi ya Gesi vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Prof.Makame Mbarawa Mnyaa.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akimkabidhi kada wa CCM  mtungi wa gesi ya kupikia iliyotolewa na  Mbunge wa Jimbo hilo Prof.Makame Mbarawa Mnyaa kwa ajili ya kupunguza changamoto ya uharibifu wa Mazingira.

NA MWANDISHI WETU,PEMBA.

 

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwasimamia Viongozi wa Majimbo hasa Wabunge na Wawakilishi watekeleze kwa ufanisi ahadi walizotoa kwa Wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu uliopita.

 

Hayo ameyasema wakati akikabidhi vitendea kazi vikiwemo mitungi ya Gesi na Pikipiki kwa Viongozi wa jimbo la Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe.Profesa Makame Mbarawa Mnyaa.

 

Amesema CCM ipo kwa ajili ya kusimamia maslahi na haki za wananchi kwa kuhakikisha kila kiongozi aliyepewa dhamana ya kuwawakilisha Wananchi katika Vyombo vya maamuzi anatekeleza wajibu wake kwa wananchi.

 

Katika maelezo yake Mbeto,amefafanua kuwa CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao CCM itatoa kipaumbele kwa Viongozi wanaofanya kazi kwa ufanisi na walizokuwa karibu na Wananchi wao.

 

"Nakupongeza sana Prof.Mbarawa umefanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani ya CCM kwani changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili Viongozi na Watendaji wengi wa ngazi za Matawi hadi Majimbo ni ukosefu wa usafiri wa kutoka eneo moja kwenda jingine,lakini kwa busara zako leo umewapatia Pikipiki na akina mama kuwapa Gesi salama kwa ajili ya ulinzi wa miundombinu ya mazingira",alisema Mbeto.

 

Kupitia hafla hiyo ya makabidhiano ya vifaa hivyo Mbeto,aliwataka Viongozi na Wanachama kuhamasisha wananchi kujiunga na CCM kwa wingi.

 

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 amesema tayari imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 98 kwa kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Dk.Mwinyi.


Pamoja na hayo Mbeto,alimpongeza Mbunge huyo Prof.Mbarawa kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta za maji safi na salama,miundombinu ya usafiri,afya,elimu na vikundi vya ujasiriamali na kwamba viongozi wengine waige mfano huo katika kuharakisha maendeleo endelevu ya majimbo.

 

Naye Mbunge wa Jimbo la Mkoani,Prof.Makame Mbarawa,Amewapongeza wanachama wa CCM kwa kazi kubwa wanayofanya ya kukitumikia Chama kwa kujitoleo.

 

Alisema leongo la kutoa mitungi ya Gesi ni kuunga mkono kampeni ya mazingira za kuhamasisha matumizi salama ya Gesi majumbani badala ya kuni na mkaa.

 

Aidha,amesema dhamira ya kutoa Pikipiki kwa Watendaji mbali mbali wa Chama ndani ya Mkoa huo ni kuwarahisishia huduma za usafiri wakati wa utekelezaji wa Majukumu yao ya kila siku.

 

Katika hafla hiyo Mbunge huyo wa Jimbo la Mikoani ametoa Pikipiki 20 zenye thamani ya shilingi milioni 64 pamoja na mitungi ya Gesi 200 kwa ajili ya Wananchi wa Jimbo hilo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.