Habari za Punde

Na.Maulid Yussuf  Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi, Mhe Sabiha  Filfil Thani  ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kujipanga vyema kuhakikisha wananchi wenye mazingira magumu zaidi wanawasaidia kulingana na uhitaji wao.

Amesema kuna baadhi ya familia wana mazingira magumu na pia wanaulemavu hivyo ni vyema kuwasaidia kwa upana zaidi.

Akizungumza wakati wa majumuisho ya ripoti ya utekelezaji kwa kipindi cha Julai hadi machi 2024 yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara hiya Kinazini Mjini Unguja, Mhe Sabiha amesema wanatambua kuwa Wizara ina kazi kubwa katika kuwafikia jamii, hivyo ni vyema kujipanga vyema.

Aidha amewataka kuendelea kutoa taaluma kwa jamii hasa wana ndoa juu ya kujitahidi kutoachana kwani inapotokea hivyo waathirika wakuu ni watoto kwa kutopata huduma na pia kutokea kwa vitendo ya ukatili na udhalilishaji. 

Hata hivyo wajumbe wa Kamati wameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kazi kubwa waliyokuwa nayo katika kushughulikia masuala ya jamii kwa ujumla pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Mapema Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Anna Athanas Paul, akiwasilisha Ripoti ya Utekelezaji ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023,2024 kwa Kamati ya Ustawi wa Jamii amesema katika kipindi  Wizara imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ikiwemo kuendelea kuratibu suala la utoaji wa pencheni jamii kwa wazee waliotimia miaka 70 na kuendelea,  kuendelea kutoa huduma za ustawi wa jamii kwa watu wenye kuhitaji, pamoja na kutoa elimu juu ya masuala ya udhalilishaji kwa jamii.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ikiwemo kushindwa kufanya uhakiki wa wazee wapya na waliopo kutokana na ukosefu wa fedha.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto bi Abeida Rashid Abdulla amesema Wizara imepokea maagizo na  michango yote iliyotolewa na wajumbe wa kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuleta ustawi bora kwa jamii.


Na Maulid Yussuf  WMJJWW

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.