Habari za Punde

Waziri Mkuu Atoa Wito kwa Wanaotekeleza Afua za Wanawake *Awataka watumie taarifa za na takwimu za sensa kuandaa mipango yao

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wanaotekeleza afua mbalimbali za wanawake watumie taarifa na takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 katika kuandaa mipango na mikakati ya uwezeshaji wa wanawake nchini.

Mbali na hayo pia Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza wadau hao wanaotekeleza afua za wanawake waandae mipango yao kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali. “Hii ni namna bora ya kuharakisha ustawi na maendeleo ya wanawake.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo jana (Jumamosi, Mei 18, 2024) katika hafla ya utoaji wa tuzo ya Malkia wa Nguvu iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Kwa Tunza Beach jijini Mwanza.

Pia, Waziri Mkuu amesema kuanzia Julai 2024 Serikali itatoa utaratibu wa namna ya uendeshaji na utoaji wa mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Nitoe rai kwa wanawake wote na makundi ya vijana na watu wenye ulemavu wazingatie utaratibu utakaotolewa na niwakumbushe kuwa fedha inayotolewa ni mikopo siyo ufadhili hivyo wanufaika wote wawajibike kuirejesha.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutoa kipaumbele katika masuala ya uwezeshaji wa kiuchumi kwa makundi maalum ya wanajamii likiwemo kundi la Wanawake.

Amesema Serikali kwa mwaka 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo kwa riba ya asilimia saba na kufanya makubaliano na NMB yatakayowezesha wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo wanawake kupata mikopo yenye riba nafuu. 

“Ninafuraha sana kwa kuwa hamasa inayotokana na ushiriki wa Tuzo ya Malkia wa Nguvu imeendelea kuwavuta wanawake wengi zaidi na kuwafanya waongeze ubora wa shughuli wanazozifanya sambamba na kukuza biashara zao.”

Amesema anafahamu kuwa moja ya malengo ya Mradi wa Malkia wa Nguvu ni kuimarisha fursa za ajira na kuwa kichocheo muhimu cha uzalishaji wa ajira mpya. “Ninawapongeza sana kwa kuchangia jitihada za Serikali katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.”

Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya tuzo hizo kwa mwaka huu ambayo ni “weka tuweke” Waziri Mkuu amesema inaleta hamasa kwa wanawake kufanya shughuli za uwekezaji na kutoa wito kwa wanawake wote kutumia kikamilifu fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini.

“Kama mnavyofahamu Serikali imeshajenga mifumo pamoja na kushaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wazalendo.  Hivyo basi, nitoe rai kwa wawekezaji wote wa ndani wakiwemo wanawake kutumia vema fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini kama ilivyo dhamira ya Mheshimiwa Rais wetu.”

Amesema zipo fursa nyingi fursa za uchumi wa buluu lakini pia, fursa za uchumi wa kidijitali ambazo zikitumiwa kikamilifu zinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wanawake.

Kuhusu eneo la uchumi wa kidijitali, Waziri Mkuu amesema amefarijika sana kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la ushiriki wa wanawake wanaofanya biashara kupitia mitandao ya kijamii mathalani, instagram, WhatsApp, telegram na tiktok.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za Malkia wa Nguvu, Liliane Masuka alisema mradi huo unalenga kukuza na kuongeza fursa za biashara zinazoendeshwa na wanawake ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

 

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, MEI 19, 2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.