Habari za Punde

malengo mahususi ya Kigoda Cha Taaluma cha Ukombozi na Maendeleo ya Afrika cha Sheikh Abeid Amani Karume yanafanikiwa ili kuleta tija za kihistoria,

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema itahakikisha inafanikisha malengo mahususi ya Kigoda Cha Taaluma cha Ukombozi na Maendeleo ya Afrika cha Sheikh Abeid Amani Karume yanafanikiwa ili kuleta tija za kihistoria, kitaaluma na maendeleo kwa ustawi wa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo kwenye ufunguzi wa Kigoda Cha Taaluma cha Ukombozi na Maendeleo ya Afrika cha Sheikh Abeid Amani Karume huko ukumbi wa Dk. Ali Muhammed Shein, Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema, Serikali pia inatambua majukwaa kama hayo yapo mengi kwenye mataifa mbalimbali duniani na kwa majina tafauti yamesaidia kufanikisha masuala ya kitaaluma na maendeleo kupitia fani mbalimbali kwa tafiti, mijadala, maandiko na mapendekezo kwa Serikali.

Vile vile Dk. Mwinyi ameziomba taasisi binafsi na mashirika mengine ya ndani na ya kimataifa, kushirikiana na Serikali kukisaidia Kigoda hicho kiendelee kutekeleza majukumu yake.

Alisema, Mzee Abeid Amani Karume alikuwa kiongozi shujaa, mzalendo aliyejitolea kuleta uhuru na maendeleo ya Zanzibar na Afrika kwa ujumla baada yakuongoza Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964, yaliyoleta uhuru wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Zanzibar.

Akitaja Malengo ya kigoda hicho Dk. Mwinyi alisema ni pamoja na kuhifadhi, kuibua na kueneza mawazo na fikra za Sheikh Abeid Amani Karume kupitia tafiti, mijadala, makongamano, mikutano na machapisho mbalimbali, pomoja na kuendeleza ushirikiano wa ndani na nje ya Afrika ulioanzisha Sheikh Karume baada ya Mapinduzi.

Pia Dk. Mwinyi aliwanasihi wanataaluma kutumia fursa ya kufanya tafiti na kazi nyengine za kitaaluma kupitia Kigoda Cha Karume ili kustawisha taaluma zao na kuleta mchango kwa jamii ya watu wa Zanzibar kwani matokeo ya tafiti zao yataisaidia Serikali kupanga mipango yake ya maendeleo.

Wakichangia mada ya Mchango wa Marehemu Mzee Abeid Aman Karume katika siasa za Zanzibar, Tanzania na Afrika kwa ujumla, viongozi wastaafu, Dk. Jakaya kikwete, Dk. Amani Karume, Dk. Ali Muhammed shein, na Mwanasiasa mkongwe na waziri Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Steven Masato Wasira walipongeza fikra, busara na maono ya Mzee Karume kwenye ukombozi wa Zanzibar dhidi ya ukoloni na utumwa.

Dk. Jakaya Mwisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya nne kwenye hafla hiyo, aliwataka Watanzania kuzitumia fursa za Maendeleo zilizopo baina ya pande mbili za Muungano Zanzibar na Tanzania bara sambamba na kuzitunza, kuzilea, kuziimarisha fikra za Mapinduzi na Muungano zilizoasisiwa na Viongozi waasisi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Alisema, kuanzishwa kwa kigoda cha Mzee Abeid Amani Karume si heshima kwa Zanzibar pekee lakini kwa taifa zima la Tanzania na tasnia yote ya Elimu nchini.

Naye, Balozi wa Kigoda cha Mzee Karume na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya Sita, Dk. Aman Abeid Aman Karume ameipongeza Serikali kwa wazo la kuanzishwa Kigonda cha Mzee Karume ili kuzienzi, kuzitunza na kuziendeleza fikra, busara na maono ya Mzee Karume katika kuakisi Maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar kwa kurithishwa vizazi vya sasa na vinavyokuja.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya Saba, Dk. Ali Muhammed Shein alisifu uwezo wa Marehemu Mzee Karume hasa kuinua Sekta ya Elimu na utaalamu kwa Zanzibar akiwa na lengo la kuijenga Zanzibar mpya kitaaluma.

Alisema, Mzee Karume alilifanikisha hilo baada ya kutoa makundi ya Wazanzibari kuyapeleka kwenye mataifa ya kijamaa barani Ulaya na Amerika ikiwemo, Cuba, China, Bulgaria, Urusi na mataifa mengine kwa nia ya kujifunza na kurejesha Zanzibar uzoefu na Maendeleo ya teknolojia.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Abdul Gulam Hussein, Akitoa shukurani zake baada ya kutawazwa kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Kigoda cha Mzee Karume, Prof. Egiland Pius Mihanjo alisifu dhana ya Hayati Mzee Abeid Amani Karume ya “Mapinduzi daima” ni kuwa na misingi imara, misukumo na mbinu bora za kuleta Mapinduzi ya Uchumi kwa maendeleo ya Zanzibar.

Akichangia mada ya Mchango Mzee Karume katika siasa za Zanzibar, Tanzania na Afrika, Mwanasiasa Mkongwe na Waziri Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Stephen Masato Wasira, alisifu juhudi za Marehemu Mzee Karume kwa kisirikisha watu wakati wa uongozi wake hasa kwenye harakati za ukombozi wa Zanzibar hasa alipounganisha vikundi vya kijamii kuanzisha harakati za siasa kwenye miaka ya 1950 zilizofanikisha Mapinduzi ya mwaka 1964.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.