Habari za Punde

Ubalozi wa Tanzania Afrika Kusini Wakamilisha Ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo

Pretoria,Afrika Kusini.

Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini chini ya Mheshimiwa Balozi James G. Bwana ulikamikisha siku tano za ziara ya ujumbe mzito wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo. Ujumbe huo ulihusisha wakurugenzi na pia wataalamu kadhaa wa sekta hiyo waliofika nchini Afrika Kusini tarehe 15 Julai 2024 ili kukamilisha masuala ya mahusiano ya nchi hizi mbili.

Ilikuwa ziara mahususi ya kimkakati kuelekea ukamilishaji wa ushirikiano madhubuti wa serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini unaojikita katika nyanja na sekta za Elimu,Sayansi, Teknolojia na uvumbuzi. Ubalozi wa Tanzania nchini hapa ukichukua eneo muhimu la kufanikishwa kwa ziara hii yenye tija kwa Mataifa haya mawili yenye historia iliyotukuka.

Wataalamu hao kutoka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bara na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na matokeo mengineyo walifika kutekeleza mpango wa ufundishwaji Kiswahili katika Wizara ya Elimu ya awali nchini Afrika Kusini. Mpango huo unaotarajiwa kufanyika kuanzia Mwaka wa 2025,Afrika Kusini wanakusudia ufundishwaji Kiswahili kwa darasa la nne(4) hadi la sita(6) kisha darasa la Kumi (10) hadi la Kumi na mbili (12) katika shule zipatazo Tisini (90). Wastani wa shule Kumi (10) kwa kila Jimbo. Afrika Kusini Ina majimbo Tisa(9).

Mpaka sasa katika Wizara ya Elimu ya Juu vyuo vikuu viwili (2) vya Cape Town na Durban vinafundisha Kiswahili vikishirikiana na kitivo cha Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. 

Dhamira hiyo itategemeana sana na bajeti kutoka serikali ya Umoja wa kitaifa ya Afrika Kusini iliyopo madarakani hivi sasa.Kupitia mkutano huu Tanzania imesisitiza utayari wake wa kutoa mafunzo kwa waalimu watakaoandaliwa ili waje kuwa waalimu wa waalimu watakaofundisha madarasa hayo. 

Ikumbukwe kuwa sera za Afrika Kusini hazitoi nafasi za ajira za kudumu kwa raia wa kigeni wakiwemo waalimu watanzania bali vipindi vya mikataba ya muda husika na si moja kwa moja.

Hivyo pamoja na uwepo wa fursa hii na utayari wa Tanzania kukibidhaisha Kiswahili ndani ya Afrika Kusini inawezekana dhamira hiyo isitekelezeke kama inavyotakiwa kutokana na changamoto za kibajeti katika serikali ya Umoja wa kitaifa ya hapa Afrika Kusini.

Hata hivyo mahusiano yenye afya baina ya nchi mbili hizi yanaleta taswira ya ushirikishwaji na mashirikiano yenye siha Bora katika nyaja hizi za Elimu Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi. Watanzania wasomi na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine SUA,Morogoro,Chuo cha Sayansi cha Nelson Mandela, Arusha,taasisi za utaalamu wa uchunguzi Afrika za O.R. Tambo na vitivo kadhaa vya uvumbuzi wa Sayansi na Anga,Wakurugenzi kadhaa toka Kamisheni ya  Sayansi na Teknolojia,Baraza la Mitihani Tanzania,taasisi ya Elimu Tanzania wote hawa  walifika ili kubadilishana ujuzi na wenzao wa Afrika Kusini. 

IMETOLEWA na
Fortunatus Charles Kasomfi 
Halisia Swahili 
RSA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.