Habari za Punde

Mhe Othman akutana na ujumbe kutoka Kampuni ya Mtandao wa simu ya Tigo- Zantel Tanzania.


 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Sekta ya Mawasiliano ni nguzo muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Othman, ameyasema hayo leo Alhamis, Oktoba 10, 2024, huko nyumbani kwake Chukwani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipokutana na kuzungumza na ujumbe kutoka Kampuni ya Mtandao wa simu ya Tigo- Zantel Tanzania.
Mtandao huo ambao upo katika wiki ya huduma kwa wateja, sambamba na kusherehekea kutimiza miaka thelathini (30) tangu kuanzishwa kwake, wamefika kwa lengo la kumshukuru Mheshimiwa Othman, kwa juhudi zake katika kuanzishwa kwa mtandao huo hapa Zanzibar pamoja na kuwa mteja wao wa muda mrefu.
Mheshimiwa Othman, amesema mawasiliano ni maisha, huku akiwataka wanamtandao huo kujikita katika kuboresha huduma zake ili kuwafikia wananchi zaidi pamoja na kutoa huduma bora, "Sasahivi kilimo ni mawasiliano, biashara mawasiliano hata elimu ni mawasiliano, hivyo huduma zikiwa bora na maisha yatakuwa mepesi". amesisitiza Mhe.Othman.
Aidha amewakumbusha kuwa Dunia kwasasa imejiimarisha katika huduma bora za kiteknolojia ambazo Tigo- Zantel wanatakiwa kwenda sambamba nayo ili kuwafikia watu wengi zaidi duniani kama ilivyo mitandao mengine.
"Ipo haja kubwa pia kutoa Elimu ya teknolojia na nyenginezo kupitia mtandao wenu, hususan kwa watoto na vijana ili kuliweka kundi hilo eneo salama na kuenda na wakati", amefahamisha Mheshimiwa Othman.
Kwa upande wake Meneja masoko tawi la Zanzibar Bwn. Mohamed Waqid Mohamed, ameshukuru mchango mkubwa wa Mheshimiwa Othman katika kuanzishwa mtandao wa simu za mkononi wa Zantel hapa Zanzibar, pamoja na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania wote, "Nizaidi ya fakhari kwetu Tigo -Zantel kutimiza miaka hii 30 tukiwa bado tupo pamoja nawe Mheshimiwa Othman, mtu uliyelipambania hili mpaka kufikia hapa", ameeleza Mohamed ambaye amemuwakilisha Mkurugenzi wa Tigo -Zantel Visiwani hapa.
Kauli mbiu ya wiki ya huduma kwa wateja ni ' Custome Service Week, Above and Beyond'.
Kabla ya kikao hicho, Mheshimiwa Othman amekutana na kubadilishana mawazo na viongozi wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Mwenge kutoka Wete kisiwani Pemba, ikiwa ni katika hatua za kukuza na kuleta hamasa katika mchezo huo hapa Zanzibar.
Timu ya Mwenge ipo kisiwani Unguja kushiriki michezo ya Ligi Kuu ya mpira wa miguu Zanzibar.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Oktoba 10, 2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.