Habari za Punde

Kuimarisha Ushirikiano Kati ya Ofisi ya Mufti na Jeshi la Polisi Zanzibar Kwa Maslahi ya Usalama wa Wananchi na Ustawi wa Jamii

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad amekutana na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na kuzungumza masuala mbalimbali ikiwa ni kuimarisha ushirikiano kati ya ofisi ya Mufti na Jeshi la Polisi Zanzibar kwa maslahi ya usalama wa wananchi na ustawi wa jamii.

Katika mazungumzo yao huko Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Mazizini, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Hamad amemuomba Mufti Mkuu wa Zanzibar kutumia Ofisi ya Mufti Kuelimisha waumini juu ya umuhimu wa kufuata sheria na kuheshimu mamlaka za kiserikali.

Amesema ni vyema kuwepo na Ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa kidini na Jeshi la Polisi katika kukemea tabia za kihalifu kama vile matumizi ya dawa za kulevya, ulevi na wizi sambamba na Kuelimisha waumini kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na matumizi ya uvaaji wa kofia ngumu, kuwa na leseni ya udereva na kuendesha magari bila ya kutumia vilevi.

Aidha, ameshauri kuwepo na mpango wa kutoa elimu kwa wafungwa na watu waliomalizia vifungo vyao Gerezani kuwafundisha maadili mema na kutorudia tena makosa waliyofanya.

Nae  na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na kulitaka kuongeza bidii katika kulinda maisha ya watu na mali zao.

Sheikh KABI amelipongeza Jeshi hilo kwa kuwa na miundombinu mizuri ya kutunza Amani ya nchi ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vimesaidia jamii kuomdokana na vitendo vya kihalifu.

Imeandaliwa na:

Kitengo cha Habari,

Makao Makuu ya Polisi,

Zanzibar

28/11/2024

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.