NA MAULID YUSSUF WMJJWW.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Juma amesema Mswahili anayejua lugha yake hana budi kufahamu mambo mengine yanayofungamana na Mswahili.
Mhe. Riziki ameyasema hayo katika sherehe za Usiku wa Mswahili uliofanyika tarehe 9/11/2024 katika Hoteli ya Methu Havana nchini Cuba, amesema ni lazima kuzingatia katika kuweka mikakati ya kuenzi na kuendeleza utamaduni wa Mswahili.
Amesema Lugha ya Kiswahili ina utamaduni wake hivyo, wanapopigania kukikuza na kukiendeleza Kiswahili duniani kote, wasisahau kufungamanisha na utamaduni wa Mswahili, na kujivunia Kiswahili kwani ni lugha ya Kiafrika isiyo na vinasaba vya lugha za kigeni.
"Lugha ya Kiswahili imepata hadhi kubwa Kitaifa, Kikanda na Kimataifa na kwa kuwa Afrika ndiyo nyumbani kwa Kiswahili, hatuna budi kuonesha kwa vitendo kuwa kweli Kiswahili asili yake ni Afrika" amesisitiza Mhe.Riziki.
Aidha Mhe. Riziki amesmea tangu kuzinduliwa kongamano la Kiswahili nchini Kuba, wamekuwa na wakati mzuri wa kujadili maendeleo ya Kiswahili ambapo ni matumaini yake kuwa wamejifunza mambo mengi ya Kiswahili katika kusaidia kukikuza duniani kote na kutoa wito kwa wataalamu na wadau wa Kiswahili kufanyia kazi yale yote waliyojifunza kutokana na Makala mbalimbali zilizowasilishwa.
Amesema tukio la usiku wa Mswahili, limejikita katika kuonesha utamaduni wa Mswahili na namna anavyotumia vitu mbalimbali vya kiutamaduni yakiwemo mavazi, vyakula, sanaa na mambo mengine mengi, hivyo kutokana na mazingira wamechagua kuwa na onesho la Khanga ambalo limekuwa vazi maarufu kwa jamii za Waswahili hasa wa Afrika Mashariki.
Amesema Kanga kwa Mswahili si vazi tu bali lina dhima mbalimbali mfano kumnasihi mtu, kumwelimisha, kumwadabisha, kutatua mgogoro na mambo mengine mengi ya hadhara na yasiyo ya hadhara.
Amesema, mkusanyiko huo wa usiku wa mswahili unawapa nafsi ya kujikumbusha dhima ya kanga katika jamii zao pamoja na kuona uvaaji wa kofia kwa kina baba Waswahili ambao nao huvaa kofia kutoa ujumbe fulani kwa walengwa.
Amefahamisha kuwa mawasiliano hayo kati ya mvaaji na mtu anayelengwa hutolewa kwa njia hiyo ya picha ambapo amesema uko umuhimu mkubwa vitu hivi kuandikwa, kwani kizazi kinapita na wasipohifadhi katika maandishi vitakuja kupita na kizazi kijacho kisijue chochote.
Hata hivyo amewapogeza waandaji wa tukio hilo la ucku wa Mswahili na kuwataka kuendelea kuburudika na kufurahika katika kukikuza kiswahili Duniani kote.
No comments:
Post a Comment