Na Maulid Yussuf WMJJWW. DAR ES SALAAM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kote nchini kujipamba na tabia njema na kufuata sunna na mwenendo wa Mtume Muhammad (S.A.W), kwani yeye ndie kigezo chema kutoka kwa Mwenyeezi Mungu.
Mhe Riziki ameyasema hayo wakati wa Sherehe ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyoandaliwa na Masjid Akram iliyopo Mbezi beach, Jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ni wajibu wa kila mmoja kufanya hivyo kama ilivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu katika aya za Qur.aan tukufu, pamoja na hadithi mbalimbali za Mtume wake Muhammad (S.A.W).
Amesema ni vyema kuhimizana kila mmoja kuwa na maadili mema, kwani jamii yenye maadili mema ndio jamii yenye uwezo wa kuishi kwa amani, umoja, maelewano na mshikamano wa kweli kwa sababu hayo yote yanakwenda sambamba na tabia njema ambazo Mtume Muhammad (S.A.W) amehimiza kushikamana na tabia hizo.
"Naomba nitoe wito kwetu sote tuliopo hapa na wale wanaotuskiliza kupitia vyombo vya habari tujipambeni na utamaduni wa kuamrishana mema na kukatazana mabaya ili nchi yetu na Taifa letu liondokane na mabaya ikiwemo rushwa, wizi, vitendo vya ukatili na udhalilishaji hasa kwa wanawake na watoto na mengineyo yaliyokatazwa na dini yetu" amesisitiza Mhe.Riziki.
Aidha amewataka kina mama kuwaangalia na kuwafuatilia kwa karibu zaidi watoto wao ili kuwakinga na vitendo vya udhalilishaji kwani tatizo hilo ni kubwa na limekuwa likiiathiri jamii hasa kwa wanawake na watoto ambao ni viongozi wa Taifa la kesho.
Mhe. Riziki ametumia fursa hiyo kuwaomba wanawake kuzidi kushikamana na kujiendeleza kielimu na kiuchumi sambamba na kusimamia wajibu wa kuilea jamii katika misingi na maadili mema kwani mwanamke ndio jamii na ndio kioo katika familia na kuimarika kwa mwanamke ndio kuimarika kwa jamii.
Mhe.Riziki amewapongeza wanawake wa Masjid Akram kwa kuanzisha Idara yao maalumu ya wanawake wa Masjid ambayo inajiongoza wenyewe pamoja na kuamua kufanya mambo mengi mazuri ya kudarsishana wao wenyewe, kusaidia Mayatima pamoja watu walioko katika mazingira magumu, jambo ambalo ni kubwa na ni la kupigiwa mfano.
Hata hivyo
Ameiomba Misikiti mengine kote nchini kuiga jambo hilo jema kwa kuwapa nafasi wanawake kuanzisha Idara kama hiyo na kujiongoza wenyewe ili kufuata miongozo ya masuala ya kheir na kukatazana mabaya.
Pia amewaomba kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini na kushikamana kuwa kitu kimoja ili waweze kuendelea kuijenga nchi na kuleta maendeleo ya haraka kwa maslahi ya Taifa na vizazi vyao.
Hata hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwaombea dua na kuwaunga mkono viongozi wa nchi Dr. Samia Suluhu Hassan na Dr. Hussein Ali Mwinyi ili wazidi kuendelea kuongoza katika hali ya amani umoja na usawa, na Taifa lizidi kubaki katika amani siku zote.
Akisoma Risala ya Maulid Hayo Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake wa Masjid Akram Ukhti Mwajuma Kingwande amesema Masjid hiyo imekuwa ikiadhimisha mazazi ya Mtume Muhammmad (S.A.W) kila mwaka na maadhimisho hayo Kwa mwaka huu ni ya 20.
Amesema pamoja na kusherehekea mazazi yake, lakini pia lengo lake ni kuwafahamisha kizazi cha sasa kumjua Mtume Muhammad (S.A.W) ili nao waweze kuwafundisha vizazi vijavyo ili kujenga Taifa lenye hofu ya Mwenyezi Mungu kwa kumtegemea yeye pekee.
MWISHO
No comments:
Post a Comment