Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, utamaduni na Michezo, wanamazoezi na wananchi waliojitokeza katika Bonaza la Afya lililoandaliwa na Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Mulid Mwita kwa kushirikiana na TAMSA SUZA lililofanyika katika Viwanja vya Kizingo Mjini Unguja.
Makamu wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kufanya mazoezi ni muhimu katika kujenga afya ya mwili na akili na kupunguza wimbi la ongezeko la maradhi yasiyoambukiza.
Ameyasema hayo katika Bonaza la Afya lililoandaliwa na Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Mulid Mwita kwa kushirikiana na TAMSA SUZA lililofanyika katika Viwanja vya Kizingo Mjini Unguja.
Amesema bonaza hilo la Afya litatoa fursa kwa Wananchi kupima afya ikiwemo sindikizo la damu, kisukari, macho, masikio, meno pamoja na zoezi la uchangiaji damu ili kuweza kuokoa maisha ya watu wanaopatwa na majanga mbali mbali ambayo huhitaji uchangiwaji wa damu kwa haraka.
Makamu wa Pili wa Rais amesema zoezi la upimaji wa afya litakuwa la siku mbili hivyo, amewaomba Wananchi kujitokeza kwa wingi katika kupima afya zao ili kuweza kupata huduma za Matibabu bure kwa wale watakaogundulika na tatizo lolote la kiafya.
Mhe. Hemed ameupongeza Uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana , utamaduni na michezo kwa kuandaa Bonanza hilo ambalo linawashajihisha wananchi kuwa na muamko wa kawaida kupima afya zao na kufanya mazoezi ili kujiweka imara kimwili na kiakili.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amevishukuru vikundi mbali mbali vya mazoezi chini ya Chama cha mazoezi ya viungo zanzibar kwa kuendelea kuiunga mkono serikali ya mapinduzi ya zanzibar katika kuamsha hamasa nchini juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi.
Sambamba na hayo Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya Afya kwa kujenga Hospitali na vituo vya Afya kuanzia ngazi ya msingi ili kuwasogezea wananchi huduma za Afya karibu yao na kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa huduma za afya kwa Wananchi wote.
Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema bonaza la Afya lina lengo la kuwashajihisha wananchi kupima afya zao kwa hiari ambapo watapata fursa ya kupima maradhi mbali mbali na kupatiwa matibabu kwa wale watakaobainika na matatizo ya kiafya.
Mhe.Tabia amesema wamepata mashirikiano makubwa kutoka Wizara ya afya hivyo, wale wote watakaohitaji matibabu makubwa zaidi watapatiwa rufaa katika Hospitali Za Wilaya na Mkoa.
Amemuomba Makamu wa Pili wa Rais kuendelea kuwashauri na kuwaunga mkono katika harakati mbali mbali za kimaendeleo kwa maslahi mapana ya Nchi yetu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) Ndugu Said Suleiman Said amewataka wananchi hasa wanamazoezi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kufanya mazoezi wakiwa salama kimwili na kiakili.
Said amesema watu wengi wamekuwa na hofu ya kupima afya zao jambo linalopelekea kuongezeka kwa maradhi mbali mbali yakiwemo maradhi yasiyo ya kuambukiza.
Bonanza hilo limetanguliwa na matembezi yaliyoanzia Skuli ya Kiembesamaki na kumalizia viwanja vya kizingo, na kufuatiwa na mazoezi ya viungo, karati, na kupambwa kwa sanaa mbali mbali ikiwemo ngoma ya kibati na mziki wa kizazi kipya.
..................
KITENGO CHA HABARI (OMPR)
No comments:
Post a Comment